MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga (Wakiwa pichani) ya Dar es Salaam amejibu hoja za wazee wa klabu hiyo kupinga kuajiriwa kwa Mkenya, Patrick Naggi kwamba si mwanachama wa klabu hiyo kwa kusema watu wengi wameajiriwa na klabu hiyo wakiwa si wanachama na kupewa uanachama baadaye.
Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam leo, Sanga alisema kwamba pia ni vigumu kutambua kwa haraka nani ni mwanachama na nani si mwanachama kwa kuwa klabu imetoa kadi nyingi za uanachama katika siku za karibuni na nyingi amezisaini yeye mwenyewe.
Sanga amemtolea mfano kocha Mkuu wa klabu, Mholanzi Ernie Brandts aliajiriwa akiwa si mwanachama na akapewa uanachama baadaye.
Pamoja na hayo, Sanga amekanusha habari kwamba Yanga imekwishamuajiri Ofisa huyo Mtendaji Mkuu wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya (FKL) na kusema kwamba mchakato huo bado unaendelea na watu wengi wamejitokeza.
Sanga amesistiza nia ya Kamati ya Utendaji kutaka kuboresha Sekretarieti ya klabu kwa kuwa hayo ni maazimio yao katika kuiboresha klabu kwa ujumla iwe na mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja.
Kuhusu mustakabali wa aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako, Sanga alisema naye yumo katika mchakato wa wanaoomba ajira Yanga na hatima yake itategemeana na matokeo ya mchakato huo, unaoendeshwa na kampuni waliyoipa tenda.
“Moja ya maazimio makubwa ambayo klabu ya Yanga sisi kama viongozi tulikubaliana, ni kuona kwamba tunaiboresha Sekretarieti yetu na kuona kwamba inaendana na uboreshaji wa timu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunakuwa na mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja,”.
“Na kwa hali hiyo, tulikubaliana katika Kamati ya Utendaji kwamba kuna nafasi kadhaa katika klabu yetu zinatakiwa kuimarishwa, ikiwemo ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mkurugenzi wa Fedha, na kwa ujumla Sekretarieti nzima kwa ajili ya kuifanya iwe katika ubora unaostahili,”.
Sanga alisema kwamba waliona ingekuwa vigumu kwa zile nafasi kutangazwa kwenye magazeti na Kamati ya Utendaji ikaona njia nzuri ni kutafuta kampuni ya uwakala kwa ajili ya kutafuta wafanyakazi, iendeshe mchakato huo kwa ajili ya Yanga.
“Kwa hiyo kuna kampuni ambayo tuliingia nayo makubaliano, kututafutia wafanyakazi wa klabu ya Yanga ambayo ilianza mchakato wa kutuletea watu mbalimbali. Lakini labda niseme, kitu kimoja kilichokuwa kimejitoeza zaidi ni kwamba tukiwa ndani ya mchakato huo, mmoja wa watu ambao walikuwa wanawania nafasi mojawapo (Naggi) ilijitokeza kwamba alifika klabu,”.
“Na tukapata taarifa alipofika kulikuwa kuna mahojiano na watu wa hapa (klabuni) kuweza kujua uhalali wake wa kufika hapa, jambo hilo sisi wengine hatukuwepo kwa hivyo hatujui nini kilichojiri, hali ambayo ilisababisha taarifa mbalimbali kutolewa na vyombo vya habari,”.
“Lakini mimi nimesimama hapa kwa niaba ya Kamati ya Utendaji kusema kwamba watu wengi wamejitokeza na mchakato haujakamilika, umefikia kwenye hatua mbalimbali. Kwa bahati mbaya tu imepokelewa vibaya na tofauti na kutangazwa kwamba tayari Yanga imekwishampata mtu fulani, jambo ambalo halikuwa sahihi,”alisema.
Jana, Baraza la Wazee la Yanga lilifanya Mkutano na Waandishi wa Habari kupinga kuajiriwa kwa Naggi, kwa kuwa si mwanachama na kusema klabu hiyo ina watu wengi wenye sifa za kufanya kazi hiyo.
Jioni ya jana, Kamati ya Utendaji ya Yanga ilifanya kikao kujadili hoja za wazee hao na haya ndiyo majibu yao.
Ilielezwa kwamba Naggi alipofuka klabuni wiki hii alifukuzwa na wanachama wakidai hawamtambui, ingawa mwenyewe alisema amekwenda kutembea tu katika klabu hiyo ili kujionea ilivyo.