Winga Mrisho Ngasa alifunga goli lake la kwanza tangu arejee Yanga na
akampikia jingine Didier Kavumbagu wakati alipoiongoza klabu yake hiyo
ya Jangwani kushinda 2-0 dhidi ya timu ngumu ya Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Ngasa aliyekuwa akicheza mechi yake ya pili
Yanga tangu amalize kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi sita kutokana
kusaini mkataba ambao alioukana na Simba, alihitaji dakika tano tu za
kwanza jana kuifungia Yanga goli la kuongoza.
Aliwainua vitini
mashabiki wa klabu hiyo ambayo amekuwa akisema anaipenda kutoka moyoni,
baada ya kufunga kwa shuti la mguu wa kushoto akimalizia mpira mrefu
uliopigwa na beki Kelvin Yondani ukababatizwa na mshambuliaji Mrundi
Didier Kavumbagu kabla ya kumfikia mfungaji ndani ya boksi ambaye
alimlamba chenga kipa wa Mtibwa, Hussein Shariff 'Casillas', na kufunga
katika lango tupu.
Yanga ambayo ilianza msimu kwa kusuasua
ikitoka sare tatu mfululizo na kupoteza mechi moja katika mechi sita za
kwanza, ilionyesha kuwa imedhamiria kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara kwa kuendelea kulishambulia lango la Mtibwa mfululizo.
Mfungaji
bora wa Yanga kwa msimu uliopita, Kavumbagu alipoteza nafasi muhimu
kuifungia timu yake goli la pili wakati shuti lake lilipogonga nguzo ya
lango akiwa ndani ya boksi.
Dakika sita baadaye, Kavumbagu
alirekebisha makosa yake kwa kuifungia Yanga goli la pili akimalizia kwa
mguu wa kulia krosi murua ya nyota wa timu ya taifa (Taifa Stars),
Ngasa.
Mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza alikosa goli la wazi akiwa
ndani ya sita wakati akiunganisha krosi bomba ya Mtokea benchi Nizar
Khalfani katika dakika ya 68 na kipa wa Yanga, Ali Mustapha 'Barthez'
alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la mtokea benchi Juma Luizio
kufuatia kona ya dakika ya 78.
Kocha wa Mtibwa Mecky Mexime alisema timu yake iliponzwa na kujisahau kwa
Inatoka uk. 24
mabeki katika dakika 25 za kwanza na akawalaumu washambuliaji wake kwa kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Ushindi
umeifanya Yanga kukwea hadi nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na
pointi 12, tatu nyuma ya vinara Simba baada ya zote kucheza mechi saba.
Katika mechi nyingi iliyochezwa jana, Prisons iliifunga Mgambo 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Vikosi
vya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jana; Yanga: Ali Mustapha 'Barthez',
Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani,
Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamisi
Kiiza na Mrisho Ngasa.
Mtibwa: Hussein Shariff 'Casillas',
Hassan Ramadhan, Paul George, Salvatory Ntebe, Salim Abdallah, Shaban
Nditi, Ally Shomari, Awadh Juma, Mussa Mgosi, Shabani Kisiga na Vincent
Barnabas