Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF (jina linahifadhiwa) alisema jijini jana kuwa, hawakuzingatia misingi ya kikatiba badala yake walitumia busara zaidi kumtaka Rage aitishe mkutano huo.
"Kufanya hivyo, si sahihi kwani iliingilia majukumu ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo ni wazi kwamba ndiyo iliyopaswa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo kikatiba.
"Rage anaweza kuwa sahihi kutokana na Katiba ya Simba inavyomuongoza, na suala hilo lilipaswa kujadiliwa kwanza kabla ya rais kutoa maagizo hayo," alisema mjumbe huyo huku akiomba hifadhi ya jina lake.
Kwa upande wa Malinzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana jijini siku hiyo, ilimtaka Rage kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura wa klabu ndani ya siku 14, lakini Mbunge huyo wa Tabora Mjini amepuuza agizo hilo kwa madai kuwa halikuzingatia Katiba ya Simba na TFF.
Akizungumza katika mahojiano maalum kwenye Ofisi za wizara yenye dhamana ya michezo jijini Dar es Salaam jana asubuhi, Malinzi alisema ameshangazwa na kauli hiyo ya Rage kutotii agizo la TFF, hivyo anasubiri barua rasmi ya mwenyekiti huyo kabla ya kumchukulia hatua stahiki.
"Sisi (Kamati ya Utendaji ya TFF) tulimwagiza aitishe mkutano mkuu, kama amekaidi hilo ni suala jingine. Tunasubiri siku 14 zimalizike na baada ya hapo, tutajua cha kufanya," alisema Malinzi.
"Kwa sasa tunalazimika kusubiri siku hizo 14 zitimie kwa sababu bado hajatupa barua rasmi ya kukataa kutii agizo la TFF. Tunasikia, kuona na kusoma habari zake kwenye vyombo vya habari," alisema zaidi Malinzi.
Alisema Kamati ya Utendaji iliamua kutoa agizo hilo baada ya kubaini kuna mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha Rage, na nyingine kutoka kwa mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa kwake.
Awali Malinzi alisema uamuzi wa TFF ulifanywa kuzingatia Ibara 1 (6) cha Katiba ya Simba kinachosema; "Simba SC ni mwanachama wa TFF, itaheshimu katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF, CAF na Fifa na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake".
Hata hivyo, Rage alinukuu Ibara ya 22 ya Katiba ya Simba inayosema "mwenyekiti wa klabu anaweza kuitisha mkutano mkuu wa dharura kwa kushirikiana na kamati ya utendaji kama anaona inafaa kufanya hivyo". Jambo ambalo alisema haoni sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa alichaguliwa agenda na kupangiwa muda.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura aliliambia gazeti hili kwa simu akiwa Nairobi jana kuwa: "Hadi naondoka ofisini (TFF) nilikuwa sijaona barua ya Rage. Mtafute Kawemba (Saad) nimemwachia ofisi."
Alipotafutwa na mwandishi jana Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba ambaye ameachiwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF, alisema bado hawajapokea barua ya Mwenyekiti wa Simba kuhusu kukataa kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa klabu.
Je, Kamati ya Utendaji ya TFF iliamua kufanya hivyo kwa sababu kabla ya hapo shirikisho hilo halikuwa na kamati hata moja ndogo baada ya Malinzi kutangaza kuzivunja kamati zote mara tu baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya Rais wa TFF Oktoba 27, mwaka huu?
Mfano
Mapema mwaka huu baada ya Malinzi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Wambura kuliomba Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liingilie kati mchakato wa uchaguzi Mkuu wa TFF uliopita, shirikisho hilo la kimataifa lilituma ujumbe maalum nchini Aprili 16, mwaka huu kufanya uchunguzi wa madai yao.
Ripoti ya ujumbe huo ilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya Fifa kilichofanyika Jumapili Aprili 28, mwaka huu na maamuzi yake kutumwa TFF Jumatatu Aprili 29 kwa barua rasmi iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke.
Ndiyo, walivyopaswa kufanya TFF kwa kuunda tume maalum ya kufuatilia suala la Simba na baadaye ripoti yake ingejadiliwa kwenye Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya shirikisho.
Rage alisema juzi kuwa 'maagizo ya uongozi mpya wa TFF hayatekelezeki' kwa vile shirikisho hilo lilipaswa kutoa adhabu kwa 'wanamapinduzi' waliokutana Jumatatu jijini Dar es Salaam na kumsimamisha kinyume cha Katiba ya Simba Ibara za 22 na 28 (Muundo wa Kamati ya Utendaji ya Simba na mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura) na Katiba ya TFF Ibara za 31 na 73 (wajumbe wa kamati ya utendaji na makosa ya kimaadili).