KIUNGO Yaya Toure anaamini Manchester City inaweza kuvunja rekodi ya mabao ya msimu katika Ligi Kuu England msimu huu.
Kiungo huyo wa nguvu amempa jeuri kocha Manuel Pellegrini juu ya uwezo wa kushambulia unaoleta matumaini ya taji kwa kusema rekodi ya Chelsea iko hatarini.
Na baada ya timu ya Pellegrini kufikisha mabao 34 wakiifunga sita Spurs Jumapili, Toure amesema lengo ni kuvunja rekodi hiyo.
Alipoulizwa kwamba inaezekana kuipiku rekodi ya Chelsea, alijibu: "Natumaini hivyo — tuna washambuliaji. Watu wawili mbele (Alvaro Negredo na Sergio Aguero) hawa watu huwezi kuamini. Wanajiamini sana.
"Lakini si kwa sababu ya wachezaji hao wawili tu. Ni timu nzima. Tunashambulia sana na washambuliaji wote wanafurahia hii. Hata (Edin) Dzeko na (Stevan) Jovetic.
"Timu inaelekeza nguvu zake katika kushambulia. Ni babu kubwa. Na unaposhinda kama tulivyofanya kwa Tottenham ni nzuri. Ni washindani wa kweli katika mbio za taji la Ligi Kuu mwaka huu,".