WAKULIMA katika kijiji cha Matuli kilichopo Mdaula kata ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamemtaka rais Jakaya Kikwete kuwasaidia kuwaondoa wafugaji wa kabila la Wamasai wanaoingiza ng'ombe zao mashambani mwao na kusababisha hasara kubwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika kijijini hapo, baadhi ya wakulima wamesema kuwa kitendo cha wafigaji hao wa kabila la wamasai kupeleka ng'ombe zao katika mashamba yao ni uvunjifu mkubwa wa amani uliopo kijijini hapo.
Mmoja kati ya wakulima hao aliyejitambulisha kwa jina la Said amedai wakulima kijijini hapo wanaihsi kwa kutegemea mazao ikiwemo mahindi pamoja na mtama pia hulkima mbogamboga, lakini wamasai bila kuogopa sheria wameamua kuvamia mashamba yao na kulisha mifugo yao.
Wanadai wameshapeleka mashitaka yao kwa uongozi wa kijiji lakini majibu hayajapatikana, 'Viongozi wa kijiji wanakaa kimya na sasa wafugaji wamevamia hadi kwenye makazi yetu na kushambulia mazao yetu ikiwemo mboga mboga', alilalamika Said ambaye aliwahi kushambuliwa na wamasai baada ya kutaka kuwafukuza katika shamba lake.
Wafugaji hao wa kimasai wamekuwa wakitumia nguvu na ubabe huku wakidiriki kutoa rushwa kwa uongozi wa kijiji ili kupitisha ng'ombe zao mashambani, aidha wakulima wamemuomba rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye aliwahi kuwa mbunge wao kuingilia tatizo hilo kwa harufu ya vita baina yao na wafugaji inaweza kutokea.
'Tunnamuomba Kikwete aingilie kati mgogoro wetu, kwani tunakoelekea si kuzuri, kuna wakati tutachoka tunaweza kupambana nao na ndio mwanzo wa vita ya wakulima na wafugaji', alilalamika mkulima huyo mwenye jazba ya kupigwa na wafugaji wakati akisaidia kuwaondoa katika shamba lake.
Jitihada za kumpata mwenyekiti wa kijiji ziligonga mwamba kufuatia simu yake ya mkononi kutopatikana huku akikosekana ofisini kwake wakati akitafutwa na mtandao huu kuelezea kwa kina matatizo hayo yanayopelekea kutokea kwa ghasia.