come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

IVO MAPUNDA AMTETEA KASEJA, AMSHANGAA KUTOMPA MKONO.

Kipa  wa Simba ambaye ni mkali wa kupangua mikwaju ya penalti, Ivo Mapunda amemtetea kipa wa Yanga, Juma Kaseja kwa kufungwa mabao mawili 'laini' katika mchezo wa 'Nani Mtani Jembe' uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi, lakini akamshangaa kwa kumsusia kumpa mkono.

Kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Kaseja aligoma kumpa mkono Ivo wakati wachezaji wa timu zote mbili wakisalimiana mbele ya Mgeni Rasmi wa mchezo huo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe ambaye alikuwa amefuatana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamali Malinzi na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe. 

Akizungumza mara tu baada ya mchezo huo kumalizika huku 'Wanajangwani' wakijawa na nyuso za huzuni, Ivo alisema hakutarajia kufanyiwa hivyo na Kaseja kwa vile hawajawahi kuwa na ugomvi wowote.


"Soka ni sehemu nzuri ya kukutanisha watu, nimekutana na Kaseja uwanjani na nilitegemea atanipokea vizuri kama Mtanzania na mchezaji mwenzake, lakini amenishangaza sana kwa kuninyima mkono," alisema Ivo.

"Sijawahi kutukanana wala kuwa na mgogoro wowote na Kaseja.

Alichokifanya ni picha mbaya kwa wapenzi wa soka, hasa watoto ambao wanatuangalia sisi (wachezaji) kama kioo chao," aliongeza Ivo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa nchini Kenya kwa kudaka mikwaju ya penalti akiwa na mabingwa wa soka wa nchi hiyo, Klabu ya Gor Mahia huku taulo zake mbili ambazo hupenda kuziweka juu ya nyavu baadhi wakizihusisha na imani za kishirikina.

Mapema katika kipindi cha pili cha mchezo wa juzi, refa wa kati aliyechezesha mchezo huo, Ramadhan Ibada kutoka Zanzibar alilazimika kuzishusha nyavu taulo hizo na kuziweka chini kwa kutokana na Ivo kuzianika juu ya nyavu la lango la Kusini la Uwanja wa Taifa.

Simu ya Kaseja, ilikuwa ikiita bila kupokewa alipotafutwa na NIPASHE jana kuzungumzia kitendo chake cha kumnyima mkono Ivo.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Mdenmark Kim Poulsen alilazimika kumtema Kaseja katika kikosi chake kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji nchini Kenya mwaka huu huku akimtumia Ivo kama kipa chaguo la kwanza.

Mara tu baada ya mchezo huo kumalizika na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali alikaririwa na vyombo vya habari akimlalamikia Kaseja kufungwa mabao rahisi huku akiweka wazi kwamba uongozi wa 'Wanajangwani' ulifanya makosa makubwa kumsajili tena kipa huyo.

Lakini Ivo alisema ni jambo la kawaida kipa mzuri kufungwa mabao kama hayo, kikubwa ni kujipanga kusahihisha makosa.

"Sijashangazwa na hali iliyomkuta Kaseja leo (juzi) uwanjani, najua ameumia sana hasa ukizingatia mabao mawili, la kwanza na la tatu yalikuwa mepesi.

Lakini ni jambo la kawaida kipa mzuri kama yeye kufungwa mabao hayo kwa sababu katika uzoefu wangu makipa wazuri kina Buffon na Heart (Joe) wamewahi kufungwa mabao mepesi kama hayo," alisema Ivo.

"Ninachoshauri wapenzi wa soka nchini, hasa mashabiki wa Yanga walichukulie kama jambo la kawaida tu, wasitafute mchawi.

Makipa wazuri wakati mwingine hufungwa mabao rahisi sana," aliongeza Ivo ambaye ametua Simba katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo kilichofungwa Desemba 15, mwaka huu.

Kaseja alionekana akitiririkwa na machozi baada ya kipyenga cha mwisho cha refa Ramadhan Ibada kutoka Zanzibar kupulizwa huku mchezaji 'kiraka' wa Yanga, Mbuyu Twite akimfuata na kumtuliza.

Tayari uongozi wa Yanga umeshamtetea kipa huyo na kusema haukumsajili mlinda mlango huyo wa zamani wa Simba ili  kuwakomoa Simba kwa kuwafunga, bali kuisaidia Yanga katika mashindano ya kimataifa.