come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KILL STARS YAPIGWA 1-0 CHALENJI, SASA KUCHEZA NA ZAMBIA MSHINDI WA TATU.

TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imefungwa 1-0 na Kenya ‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, ikisindikizwa na mvua.

Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu keshokutwa mchana Uwanja wa Nyayo tena, wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Thiery Nkurunziza wa Burundi, aliyesaidiwa na Idam Hamid wa Sudan na Mussie Kinde wa Ethiopia, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na kumchungulia kipa Ivo Mapunda.


Baada ya bao hilo, Stars walizinduka na kuanza kushambulia, lakini ukuta wa Kenya ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote.

Nafasi pekee nzuri ambayo Stars waliipata ilikuwa dakika ya 44, wakati kona nzuri ya Mrisho Ngassa ilipopanguliwa na kipa Duncan Ochieng, lakini Mbwana Samatta akachelewa kuunganisha, Joackins Atudo akaondosha kwenye hatari.

Kipindi cha pili Stars ilicheza vizuri zaidi, lakini bado ukuta wa Harambee ulikuwa mgumu na nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho ilikuwa dakika ya 88, wakati Mbwana Samatta alipomtoka beki wa Kenya na kuingia vizuri ndani ya 18, lakini akapiga juu.

Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa wakilia na ikabidi viongozi wachukue jukumu la kuwabembeleza. Nahodha Kevin Yondan ndiye alikuwa ana hali mbaya zaidi.

Kikosi cha Stars leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Michael Pius, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Hassan Dilunga/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk65, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Amri Kiemba/Farid Mussa dk65.

Kenya; Duncan Ochieng, Allan Wanga/Noa Wafula dk81, James Situma, Aboud Omar, Joackins Atudo, Peter Opiyo, Francis Kahata, Anthony Akumu, Clifton Miheso/Paul kiongera dk88, David Ochieng Owino na Edwin Lavatsa.