Uongozi wa Yanga umemrejesha kundini, kiungo Athuman Iddi ‘Chuji’ aliyekuwa akitumikia adhabu ya kusimamishwa kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.
Chuji alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo kwa muda usiojulikana mwishoni mwa mwaka jana baada ya kudaiwa kuondoka vyumbani na kutimkia nyumbani kabla ya mchezo wa Nani Mtani Jembe kati ya Yanga na Simba kumalizika.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema jana kuwa, Chuji amesamehewa baada ya kuandika barua ya kuomba msamaha na kukiri kosa na kuahidi kutorudia tena kufanya kitendo hicho.
“Tumemrejesha kundini Athumani Iddi aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu ambapo aliondoka vyumbani kabla ya mchezo kati yetu na Simba kumalizika,”alisema Njovu.
Aliongeza:”Uongozi umefikia uamuzi huu wa kumsamehe Chuji baada ya yeye mwenyewe kukiri kosa na kuomba msamaha na kuahidi kutorudia tena kitendo hicho au kufanya kitendo kingine chochote cha utovu wa nidhamu.”
Njovu alisema, kabla ya uamuzi huo Chuji alipewa onyo kali na kupewa kipindi cha matazamio ambapo kwa kipindi cha mwezi mmoja alionekana kubadilika na kurejea katika nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.
Alisema, Chuji ataungana wachezaji wengine wa timu hiyo kesho watakaporejea jijini Dar es salaam kutoka Tanga walikokwenda kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union.