Meneja wa Machester United, David Moyes, amekubali mashataka ya shirikisho la kandanda la Uingereza, FA, la kushutumu waamuzi wa mechi.
Moyes alipandishwa mori na marefarii pale wababe hao walipochakazwa 2-1 ugenini Sunderland juma lililopita na baadaye, alikemea vikali waamuzi wahusika.
Mwalimu huyo anatizama kutozwa faini au kupewa onyo baada ya kusikizwa kwa kesi ya nidhamu.
Moyes alisema timu yake, “inacheza dhidi ya marefarii pamoja na wapinzani,” baada ya mkondo wa kwanza wa semi fainali ya kombe la League Cup ugani Stadium of Light.
Raia huyo wa Scotland alizua tashwishi kutokana na mkwaju wa adhabu ambao ulielekea kwa bao la kwanza la Sunderland na baadaye, penalti iliyochangia bao la ushindi.
Shtaka hilo linakuja wiki moja baada ya meneja wa Liverpool, Brendan Rodgers, kutoizwa faini nono ya pauni 80,000 za Uigereza baada ya kufokea refa Lee Mason katika mechi yao ugenini Manchester City Desemba 26.