Uvumi ulikuwa umeenea kwamba raia huyo wa Argentina angejiuzulu baada ya Nicola Cortese, anayetambuliwa na wengi kwa kuchangia kubadilisha Southampton na kuifanya timu kuu Uingereza, kujiuzulu Jumatano.
Lakini mwanamume huyo wa miaka 41 aliambia wanahabari kwamba amejitolea asilimia 100 kwa Southampton. "Nina wajibu wa kitaalamu kwa kila mmoja katika klabu hii, na kwa mashabiki,” akasema.
Pochettino alikuwa amedokeza mwezi mei mwaka jana kwamba angeondoka klabu hiyo ya pwani mashariki kama Cortese angegura St Mary's, lakini alifafanua sababu ya kubadilisha uamuzi huo.
“Hali ilikuwa tofauti kabisa miezi minane iliyopita, nilikuwa nikizungumza baada ya kumaliza msimu wangu wa kwanza,” alimbia kikao cha wanahabari katika uwanja wa Southampton.
“Katika katika shughuli inayofaa kufuata katika klabu hii…na nilinena na Nicola Cortese kuhusu hili … nimejitolea kwa klabu hii, wafanyakazi, mashabiki, wachezaji, jamii ya klabu hii. Haina maana yoyote kwangu kuondoka katikati ya safari hii.
"Ninataka kumshukuru sana Nicola Cortese kwa kunileta kwenye klabu hii pamoja na familia yangu. Nicola anakubaliana na uamuzi wangu wa kubaki. Alinisihi nifanye jambo moja pekee – nalo ni kujaribu kushinda Jumamosi dhidi ya Sunderland."
Mmiliki wa klabu Katharina Liebherr amechukua jukumu la mwenyekiti asiye na mamlaka makuu na kazi ya kutafuta Afisa Mkuu Mtendaji imeanza.
Pochettino alisema alikutana kwa muda mfupi na Liebherr aliyesisitiza kwamba ana imani naye.
“Nilizungumza naye kwa dakika tano na alinielezea kwamba ana imani name na wafanyakazi,” Pochettino alisema.
"Hakukuwa na wakati wa kuzungumza naye kuhusu siku za usoni. Ilikuwa tu ni kujuliana hali upesi na kuambiana kwaheri, alinijuza kuhusu imani yake.”
Pochettino alipuuzilia mbali uvumi kwamba klabu pinzani zilikuwa zikizunguka, tayari kujifaidi kutokana na msukosuko St Mary's na kutoroka na baadhi ya wachezaji nyota ikiwa ni pamoja na mchezaji mwenye kipaji adimu Luke Shaw.
"Ninataka kuweka hili wazi. Hakuna wachezaji watakaouzwa Southampton FC," akasema.
"Imani yangu haijabadilika kutoka ilivyokuwa wiki moja iliyopita. Hakuna wachezaji ninaotaka katika klabu hii watauzwa.”
Southampton wamo nambari tisa katika ligi kuu ya Uingereza yenye timu 20 wakiwa na alama 30 kutoka kwa mechi 21 walizocheza kufikia sasa – alama 18 nyuma ya viongozi.