Hatimaye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limemaliza utata baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu uhalali wa usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Yanga na kueleza kuwa SC Villa iko sahihi kumuuza nyota huyo kwa Wanajangwani.
Januari 22 mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ilisimamisha usajili wa Mganda huyo katika klabu ya Yanga wakati ikisubiri ufafanuzi wa Fifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema Fifa imejibu barua yao kuhusu uhalali wa usajili wa nyota huyo katika klabu ya Yanga na malipo ya uhamisho wake kutoka Simba kwenda klabu ya Etoile du Sahel (ESS) ya Ligi Kuu ya Tunisia.
“Fifa wametujibu masuala mawili tuliyowaomba watupe ufafanuzi. Suala la kwanza lilikuwa uhalali wa usajili ya mchezaji Emmanuel Okwi katika klabu ya Yanga ambao wamesema ni halali kusajiliwa kutoka SC Villa kwa sababu ndiyo iliyokuwa inammiliki na ndiyo iliyotoa ITC (Hati ya Uhamisho wa Kimataifa) kwa kushirikiana na Fufa (Shirikisho la Soka Uganda).
"Suala la pili lilikuwa linahusu fedha za Simba ambao wanadai malipo ya uhamisho wa mchezaji huyo kwa klabu ya Etoile, hili Fifa wamesema wanalifahamu na bado liko kwao wanalishughulikia," alisema Mwesigwa.
Alisema kuwa barua hiyo ya FIFA imeeleza kwamba kesi kati ya Simba na Etoile du Sahel ya Tunisia haimuhusu mchezaji huyo.
"Kwa kuwa sisi ndiyo tulimzuia Okwi kucheza, kuanzia leo (jana) tunatangaza kwamba Okwi ni mchezaji huru na ataanza kuitumikia Yanga," alisema Mwesigwa.
Simba haijalipwa dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 480) za mauzo ya mkali huyo wa kufumania nyavu kutoka kwa ESS tangu Januari mwaka jana ilipowauzia wawakilishi hao wa Tunisia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka huu.
LESENI YA CAF
Katibu Mkuu huyo aliendelea kueleza kuwa TFF itaisaidia Yanga kusaka kibali cha Okwi kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ili aitumikie timu yao katika mashindano yanayoendelea ya Klabu Bingwa Afrika.
"Kama Yanga bado wanahitaji kumtumia mchezaji huyo katika mashindano ya kimataifa, waje ili tuwasaidie kumwombea kibali CAF," alisema.
YANGA WANENA
Alipotafutwa na mwandishi jijini Dar es Salaam jana mchana, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema wamefurahishwa na maamuzi hayo ya Fifa na kwamba tayari mchakato wa kusaka kibali cha CAF umeanza.
"Tumefarijika sana baada ya kupata taarifa hiyo, TFF wametuandika barua leo (jana) wakitujulisha kuhusu kilichojiri na wamesema wataitaarifa CAF kuhusu kilichotokea ili itoe kibali cha mchezaji wetu kucheza mashindano ya Afrika," alisema Njovu.
BINKLEB
Ikumbukwe kuwa baada ya kusimamishwa kwa usajili wa Okwi na TFF, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb alisema kuwa walifuata taratibu zote kabla ya kunasa saini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa watani wao wa jadi, Simba na