Serikali ya Uchina imechapisha
picha zilizonaswa na mtambo wake wa satelite zikionyesha mabaki ya kitu
kipana kikielea katika bahari ya Kusini mwa Uchina.
Huku ikiwa na raia wake 154, ambao walikuwa abiria kwenye ndege hiyo ya Malaysia, serikali ya Uchina imetuma mitambo kumi ya satellite kusaidia katika harakati za kutafuta ndege hiyo.
Picha za vifaa hivyo vitatu, ambavyo moja ina upana wa takriban mita 24 kwa 22, zilichukuliwa siku ya Jumapili, siku moja tu baada ya ndege hiyo kupotea, lakini zilichapishwa siku ya Jumatano.
Picha hizo za satellite zimeweka vifaa hivyo takriban maili mia moja kutoka kwa njia iliyotarajiwa kutumiwa na ndege hiyo na sio mbali kutoka kwa kisima kimoja cha mafuta, ambako mfanyakazi mmoja aliripoti kuona kitu kilichokuwa kikichomeka angani siku ya Jumamosi asubuhi.
Lakini siku chache zilizopita, kumekuwa na fununu kadhaa kuhusiana hatma ya ndege hiyo lakini zote zimekuwa uongo.
Makundi ya uokozi hiyo vile vile wanatafuta mabaki ya ndege hiyo katika maji inayokaribiana na rasi ya Malaysia, kwa sababu wanaamini kuwa ndege hiyo ya Malaysia ilibadili mkondo na kuelekea Magharibi.