Rais wa shirikisho la mchezo wa
soka nchini Malawi, FAM, Walter Nyamilandu, amekariri kuwa timu ya taifa
ya nchi hiyo, haijajiondoa kutoka kwa mechi za kufuzu kwa fainali ya
kombe la mataifa bingwa barani, ACN, itakayoandaliwa nchini Morocco.
Lakini imesemekana kuwa serikali ya Malawi, ilikuwa imeeleza shirikisho hilo kuwa, ilikuwa na fedha zitakazotosha timu hiyo ya taifa kushiriki katika mechi hizo za kufuzu au fainali ya kombe ya taifa bingwa barani kwa vijana chipukizi itakayoandaliwa nchini Senegal mwaka wa 2015.
Lakini siku ya Jumatano, Nyamilandu, ameiambia BBC, kuwa wao hawajajiondoa na hawana nia yoyote ya kujiondoa.
Tatizo la ukosefu wa fedha sio jambo geni kwa timu hiyo ya Malawi, ambayo Septemba mwaka uliopita ilishauriwa na serikali kutoshiriki mechi yao ya kufuzu dhidi ya Nigeria mjini Calabar, kwa kuwa shirikisho hilo lilikuwa limemaliza fedha zilizotengewa na serikali.
Wadadizi wanahisi kuwa matamshi ya Nyamilandu ni ya kushinikiza serikali ili kutoa fedha zaidi kwa timu hiyo ya taifa.