MSHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta jana usiku ameifungia bao muhimu timu yake, TP Mazembe ya DRC ikilala 2-1 mbele ya wenyeji, Sewe Sport ya Ivory Coast mjini Abidjan katika mchezo wa kwanza Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wageni walitawala mchezo tangu mwanzo na mshambuliaji mwingine Mtanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu alikaribia kufunga dakika ya tano kama, kama si jitihada za kipa wa Sewe, Sylvain Gbohouo kuokoa.
Ulimwengu aliyeanza katika safu ya ushambuliaji ya Mazembe, huku Samatta akianzia benchi, alisababisha misukosuko mingi langoni mwa wenyeji, kwani dakika ya 17 aligongesha mwamba wa juu.
Lakini baada ya misukosuko hiyo, wenyeji walizinduka na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 38, mfungaji Roger Assale aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Joseph Kadjo Kameni. Na Assale alikaribia kufunga tena dakika mbili baadaye kama si kazi nzuri ya kipa wa Mazembe, Robert Kidiaba kuokoa.
Sewekes walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza bao 1-0 kabla ya kurudi kwa hasira zaidi kipindi cha pili kusaka mabao zaidi kabla ya mchezo wa marudiano mjini Lubumbashi wiki ijayo.
Kocha wa Sewe, Rigo Gervais aliwaingiza kiungo Hevra Kouassi na mshambuliaji Hermann Kouao kuchukua nafasi za Ocansey Mandela na Zadi Wawa na hiyo ikawasaidia kupata bao la pili dakika ya 82 lililofungwa na Christian Kouame kwa penalti, baada ya Roger Assale kuangushwa kwenye eneo la hatari na Jean Kasusula.
Lakini The Corbeaux walifanikiwa kupata bao la ugenini dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho kupitia kwa Samatta aliyetokea benchi na sasa Mazembe watahitaji ushindi wa 1-0 tu nyumbani Lubumbashi katika mchezo wa marudiano wikiendi ijayo ili kutinga Hatua ya Makundi.