come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: USAJILI WA OKWI HAUKUWA NA FAIDA YANGA

Na Fikiri Salum

LIGI kuu Tanzania bara imemalizika rasmi April 19 huku Yanga ikiutema ubingwa wake na kuchukuliwa na Azam fc yenye maskani yake Mbagala Chamanzi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.

Kuukosa ubingwa kwa klabu ya Yanga kumeweza kuzua mshangao mkubwa huku mamilioni ya fedha yakitumika katika kukiimarisha kikosi hicho, tayari uongozi wa Yusuf Manji umeanza kuonekana haufai mbele ya Wanayanga.

Kipi kinachopelekea mpaka kuuona uongozi huo haufai wakati amefanya mambo mengi ya maana katika utawala wake, Ni nadra sana kwa timu ya Yanga kufanya vibaya pasipo kutokea machafuko.

Imezoleleka Yanga inapofanya vibaya basi mifarakano ya hapa na pale lazima itokee na ikiwezekana mapinduzi makubwa hufanyika, lakini Manji ameweza kudhibiti hilo na Yanga ipo shwari licha ya maneno maneno ya hapa na pale kutokosekana.


Yanga ilianza ligi ya msimu uliopita kwa kishindo ambapo iliweza kuichakaza Ashanti United mabao 5-1, ushindi huo mkubwa ulipokelewa kwa furaha na Wanayanga, isitoshe Ashanti imekuwa ikitoa ushindani mkubwa inapokutana na Yanga.

Hata hivyo kasi hiyo haikuendelea sana ambapo ilijikuta inashikwa shati na Coastal Union, Mbeya City na Prisons hatimaye kujikuta inapoteza kiti chake cha uongozi na kuwaachia watani zao wakubwa katika soka la Tanzania Simba.

Simba ilikamata kiti cha uongozi mpaka pale ilipoenguliwa na Azam fc, kasi ya Yanga iliendelea tena katikati ya msimu na kushikilia tena usukani ambapo ilikuwa ikipokezana na Azam au Mbeya City timu iliyopanda daraja na kufanya kweli.

Kikosi cha Yanga kilikuwa kinanolewa na Mholanzi Ernie Brandts akisaidiwa na Fred Minziro 'Majeshi', Yanga ilikuwa tayari imeshajipangia utaratibu wake ambapo ulionekana kuwa mzuri.

Ilikuwa na kikosi imara ambapo mapema kabisa mwa msimu ilifanya usajili wa maana, Yanga ilimsajili Mrisho Ngasa aliyekuwa kwa mkopo Simba sc akitokea Azam fc, pia ilimuongeza Hussein Javu aliyekuwa Mtibwa Sugar.

Usajili huo ulienda sambamba na ule wa kipa Deogratus Munishi 'Dida' aliyemaliza mkataba Azam fc, usajili huo uliisaidia Yanga kuongoza ligi katika mzunguko wa kwanza, matokeo ya 3-3 dhidi ya Simba yaliweza kuwaudhi Wanayanga na kupelekea uongozi wa timu hiyo kutimua makocha wote.

Yanga ilimtimua kocha mkuu Brandts na msaidizi wake Minziro pamoja na kocha wa makipa na daktari wa timu, Yanga walikwenda mapumziko kujiandaa na mzunguko wa pili, timu zote 14 zilianza kujiimarisha ambapo dirisha dogo la usajili lilifunguliwa.

Yanga ilisajili wachezaji watatu ambao ni golikipa mahiri nchini na anayeheshimika sana kuliko wote Juma Kaseja ambaye aliwahi pia kuichezea miaka ya nyuma ikiwemo na Simba mbali na Kaseja Yanga ilimsajili Emmanuel Okwi na Hassan Dilunga.

Usajili wa Okwi ndiyo uliokuwa gumzo sana kwakuwa mchezaji huyo alikuwa anaichezea Simba sc na baadaye kuuzwa kwa klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia, usajili wa Okwi ulizua utata kwani awali akiwa Simba Yanga walitaka kumsaini lakini walishindwa.

Uongozi wa Simba ulimwekea ngumu nyota huyo aijiunge na Yanga, hivyo kitendo cha Yanga kumsaini akitokea SC Villa ya Uganda kiliweza kuzua utata uliopelekea shirikisho la kandanda nchini TFF kuomba ufafanuzi FIFA.

Okwi alisimamishwa kutoichezea Yanga hadi Fifa itakapotoa ufafanuzi wa kisheria juu ya uhalali wake kukipiga Yanga, Baada ya Fifa kumruhusu Okwi kuichezea Yanga, Wanayanga waliamini msimu uliopita ungekuwa kwao.

Lakini cha kushangaza mchezaji huyo hakuweza kuisaidia Yanga na baadaye alianza kuidengulia timu hiyo na baadaye kupoteza ubingwa wake, Okwi alishindwa kuisaidia Yanga kwenye michuano ya kimataifa na pia kushindwa kuibeba katika ligi kuu bara.

Kinyume na matarajio ya viongozi wa Yanga ambao walidhani usajili wa Okwi, Kaseja na Dilunga ungeweza kuleta mabadiliko, naweza kuthubutu katika usajili huo Yanga imeambulia kwa Hassan Dilunga ambaye amekuwa na msaada mkubwa katika mechi zake alizocheza za mwisho wa msimu.

Dilunga amecheza mewchi za mzunguko wa pilina kufanikiwa kumweka benchi kiungo ghali Afrika mashariki Haruna Niyonzima ambaye mpaka sasa anashindwa kuamini, Niyonzima amedumu miaka mitatu ndani ya Yanga bila kusugua benchi lakini ujio wa Dilunga umeweza kummaliza.

Okwi ameshindwa hata kuifikia kasi ya mshambuliaji Hussein Javu aliyesajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar, Javu amecheza mechi chache lakini amefunga magoli manne, tofauti na Okwi ambaye mecheza mechi nyingi na kufungamagoli mawili.

Kuna uwezekano mkubwa Yanga ikaingia hasara ili kutengeneza upya kikosi chake, Hans Van Der Pluijm Mholanzi aliyechukua mikoba ya Mholanzi mwenzio Ernie Brandts anahitaji kutengeneza kikosi imara kitakachoweza kurejesha mataji Jangwani.

Yanga ina kazi nzito kurejesha ubingwa wake wa klabu bingwa Afrika mashariki na kati pamoja na ligi kuu bara, ili iweze kufanya vizuri msimu ujao Yanga inahitaji mshambuliaji wa kati atakayesaidiana na waliopoa ambao ni Hussein Javu, Jerry Tegete, Hamis Kiiza, Didider Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Okwi mwenyewe.

Pia inapaswa kusajili kiungo wa kati atakayesaidiana na chipukizi Hassan Dilunga kwani uwezo wa Niyonzima tofauti na Dilunga hivyo anahitajika mchezaji anayefanana na Dilunga.