come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA YAMRUHUSU TAMBWE KUONDOKA

Siku  moja baada ya mshambuliaji Amisi Tambwe kutangaza nia ya kujiunga na Azam FC au Yanga, uongozi wa Simba umesema hautamzuia nyota huyo kuondoka katika klabu hiyo ya Msimbazi.

Mwishoni mwa wiki Tambwe, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14, alisema jijini Dar es Salaam kuwa yuko tayari kuondoka Simba na kujiunga na timu yoyote itakayompa 'mpunga' mwingi.

"Bado nina mkataba wa mwaka mmoja na Simba lakini timu nyingine ikija na dau kubwa niko tayari kujiunga nayo," alisema Tambwe katika mahoajiano  jijini mwishoni mwa wiki.


"Kwa sasa ni mapenzi na klabu ya Simba, lakini nikisajiliwa na Azam au Yanga, nazo nitazipenda tu," alisema zaidi raia huyo wa Burundi.

Akizungumza kwa simu jana akiwa jijini Kigali, Rwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema wako tayari kumwachia nyota huyo kujiunga na timu yoyote atakayotaka.

"Sera ya Simba iko wazi, hatuzuii mchezaji yeyote kujiunga na timu anayoitaka, kama Tambwe akipata timu itakayompa maslahi mazuri zaidi, sisi hatuna pingamizi, tutamwachia lakini wafuate tu taratibu zote za kuvunja mkataba maana bado ana mkataba na Simba," alisema Hanspope.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na michuano ya Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati -- Tambwe, alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili Agosti mwaka jana akitokea klabu ya Vital'O ya kwao Burundi.

Mkali huyo wa kufumania nyavu ameichezea Simba mechi 23 za Ligi Kuu msimu wa 2013/14 na kuifungia magoli 19.