Uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam uliopangwa kufanyika Mei 4, mwaka huu huenda ukasogezwa mbele kutokana na uongozi wa klabu hiyo mpaka sasa kutojua ni katiba ipi itatumika katika uchaguzi huo wa kupata viongozi wapya, imeelezwa.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba bado uongozi unasubiri kupata mwongozo kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini.
Kamwaga alisema baada ya kupeleka marekebisho waliyofanywa katika katiba yao na wanachama wa klabu hiyo, uongozi unasubiri maelekezo rasmi ambayo yatakuwa yameainishwa na TFF ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa chaguzi zote za wanachama wake.
"Tumeshapeleka TFF katiba yetu kwa kuweka vipengele vilivyofanyiwa marekebisho katika mkutano mkuu, bado inafanyiwa kazi, ila pia tunaendelea na maandalizi ya uchaguzi kwa kuangalia kanuni zinavyoeleza ili kamati ianze mchakato," alisema Kamwaga.
Katibu huyo alisema uongozi utahakikisha unafuata maelekezo yote muhimu ili zoezi hilo la uchaguzi litakapoanza kusiwe na upungufu wa aina yoyote.
Wiki iliyopita Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilikutana na kuamua kukiondoa kipengele kipya cha 26 cha Katiba mpya ya Simba na kurejesha kipengele cha zamani kwa maelezo kwamba kilikuwa kinapingana na katiba ya shirikisho hilo.
Habari zaidi kutoka TFF zinasema kwamba shirikisho hilo lilimuandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji, Frederick Werema, kuomba ufafanuzi juu ya kipengele hicho na inadaiwa kwamba wameelezwa kuwa mabadiliko hayo hayaendani na katiba ya nchi hivyo yanapaswa kuondolewa.
Endapo kipengele hicho kitazuiwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa kuteuliwa, Zacharia Hanspope, anayetajwa kuwania uenyekiti atakosa sifa ya kugombea kama alivyoondolewa katika mchakato wa uchaguzi uliopita.
Simba ilifanya uchaguzi wake wa mwisho 2010 na katika uchaguzi huo, Ismail Aden Rage, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo yenye makao makuu Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini. Tayari baadhi ya wanachama wameshatajwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.