Kiingilio cha chini cha mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (Flames) itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni Sh. 5,000, imeelezwa.
Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mashabiki watakaolipa kiingilio hicho ni wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani huku upande wa VIP B na C kiingilio kikiwa Sh. 10,000 wakati VIP A kitakuwa ni Sh. 20,000.
Alisema mechi hiyo ya pili kwa timu hizo kumenyana ndani ya mwezi huu baada ya kutoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya Mei 4, mwaka huu, itaanza saa 11 kamili jioni ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi zaidi kuishuhudia kwa vile itakuwa ni siku ya kazi.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, itawasili kesho asubuhi ikitoka Tukuyu, Mbeya ambako imepiga kambi yake chini ya kocha mpya Mholanzi Mart Nooij.
Flames inayonolewa na mchezaji wake wa zamani, Young Chidmozi tayari ipo nchini kwa ajili ya mechi hiyo inayotumiwa na timu zote kama sehemu ya maandalizi ya mwisho kwa ajili mechi za mchujo za Kombe la Afrika (AFCON). Flames iliwasili jana mchana kwa ndege ikiwa na msafara wa watu 27.
Wakati Stars kwenye mechi za AFCON itarudiana na Zimbabwe jijini Harare, Flames nayo itakuwa ugenini N’djamena kuikabili Chad.
Wambura alisema mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo wa marudiano wa michuano ya Afrika na Zimbabwe (Mighty Warriors) utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare.
Katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya mchujo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, Stars ilishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na inahitaji japo sare ili kutinga hatua ya pili ya mchujo.
Ikiweza kuingia katika raundi ya pili ya mchujo itakutana na mshindi baina ya Sudan Kusini na Msumbiji.
Mshindi baina yao atafuzu kwa hatua ya makundi ya kufuzu. Endapo Tanzania itatinga hatua ya makundi ya kuwania kufuzu itaingia katika Kundi F la kufuzu ambalo linaundwa na timu za Zambia, Niger, Cape Verde.
Timu mbili kutoka kila kundi la kuwania kufuzu kati ya makundi saba yaliyopo, pamoja na mshindi wa tatu mmoja aliyefanya vizuri zaidi, wataungana na mwenyeji Morocco kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco.
