Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeahidi kuzisaidia timu zinazotoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ili zifanikiwe zaidi katika soka na kuweka ushindani duniani kote.
Akizungumza katika semina maalumu iliyoandaliwa na Cecafa Jijini Dar es Salam jana, mkurugenzi msaidizi wa mawasiliano na masuala ya kijamii wa Fifa, Nicholas Maingot alisema shirikisho hilo litatoa misaada ya kifedha, kiutawala na pia kuanzisha programu mbalimbali za kuinua soka katika ukanda huo.
“Siku zote ukanda wa Cecafa umekua mstari wa mbele kuwajibika na kuhakikisha mpira wa miguu unazidi kupata umaarufu duniani. Tunashukuru kwa kujitoa huko na sisi tunaahidi kuendelea kufanya kazi bega kwa bega na shirikisho hili ili kuupa mpira umaarufu zaidi hususani kwa kutumia mawasiliano,” alisema Maingot.
Fifa kwa kushirikiana na Cecafa wanaendelea na semina ya siku mbili jijini Dar es Salam yenye lengo la kuwaongezea ujuzi viongozi wanachama wa Cecafa juu ya umuhimu wa mawasiliano kwenye soka hususani katika karne hii ya digitali. Wanachama wa Cecafa ni Burundi, Kenya, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Uganda, Tanzania na Zanzibar.
Awali semina hiyo ilikuwa ifunguliwe na katibu mkuu wa Fifa, Jerome Valcke, lakini jana wajumbe wa mkutano huo waliwekewa CD ya katibu huyo akiwaomba radhi kutohudhuria mkutano huo kwa vile wakati akijiandaa kuja Tanzania, mke wake aliumwa na uchungu na amebahatika kujifungua mtoto wa kike aliyepewa jina la Valentine.
Semina hiyo inaendelea kwenye Hoteli ya Double Tree jijini, na lengo la semina hiyo ni kujadili masuala mbalimbali ya utawala wa soka na changamoto zinazoikabili Cecafa. Pia masuala ya mawasiliano na upashanaji habari katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.