come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

TAIFA STARS V MALAWI HATUMNWI MTOTO DUKANI HUKO MBEYA

Na Mwandishi wetu, Mbeya

Taifa Stars inahitaji kusafisha nyota leo mbele ya mashabiki wa soka mkoani Mbeya na Tanzania kwa ujumla kwa kuitandika Malawi ‘The Flame’ katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Wapenzi wa soka mkoani Mbeya walianza jana kupeperusha bendera ya Taifa kila kona huku gari la matangazo likizunguka mitaani kuwahimiza wajitokeze kwa wingi kujionea mchezo huo kwa kiingilio cha Sh5,000.


Hata hivyo, mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali kutokana na ukweli kwamba timu zote zitataka kufuta machozi ya kufungwa katika mechi za kirafiki zilizochezwa wiki mbili zilizopita, ambapo Stars ilinyukwa mabao 3-1 na Burundi wakati Flame ilitandikwa 4-1 na Zimbabwe, ambao wana mchezo na Stars mwishoni mwa mwezi huu.

Kocha msaidizi wa Malawi, Jack Chamangwana alisema timu yake itacheza kwa nguvu zote ili kupata kipimo cha mwisho kabla ya kuikabili timu ya Taifa ya Chad jijini Lilongwe, wiki chache zijazo katika moja ya mechi za kuwania kufuzu kwa michuano ya Mataifa ya Afrika.

Naye kocha mpya wa Stars raia wa Uholanzi, Martinus Nooij alisema kwa kifupi wamejiandaa kuikabili Malawi kikamilifu.

Nooij alisema timu yake iliyoweka kambi mjini Tukuyu, wilayani Rungwe mkoani hapa inaendelea vizuri na ilifika juzi jijini Mbeya kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine ili kuuzoea.