Mzee Small kwa zaidi ya miaka miwili alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi, alizikwa jana katika makaburi ya Segerea na mamia ya waombolezaji wengi wao wakiwa wasanii wa fani tofauti.
Rais Kikwete aliwasili nyumbani kwa marehemu Tabata Kisiwani kunako saa 8:30 za mchana na kukaa kwa zaidi ya nusu saa akizungumza na wanafamilia kabla ya kuaga na kuondoka ili kuruhusu taratibu zingine za mazishi kuendelea.
Wakimuelezea marehemu Mzee Small ambaye ameacha mke na watoto sita mara baada ya mazishi katika makaburi ya Segerea , baadhi ya wasanii walisema kuwa marehemu alikuwa mfano mzuri na dira kwa walio wengi katika fani hiyo.
“Tutamkumbuka mwa mengi, lakini kubwa ni mapenzi katika kazi yake, aliipenda sana fani yake na alikuwa tayari wakati wote” alisema Yusuf Kaimu ‘Pembe’ na kuongeza kuwa alikutana na marehemu kwa mara ya kwanza katika kikundi cha Sanaa cha Reli kilichokuwa kinamilikiwa na Shirika la Reli (TRC) miaka ya themanini.
Pembe alisema kuwa marehemu alikuwa mcheshi na mpenda na mwenye mzaha mwingi, lakini hakuwa na simile pale unapokuwa unataka kuharibu kazi na daima alikuwa mwongozaji na rafiki wa wengi.
Ulimboka Mwakalasa ‘Senga’ alisema kuwa Mzee Small alikuwa dira ya fani yake ingawa hakuwahi kufanyakazi nao kwa muda mrefu, lakini daima alikuwa anamfuata nyuma katika kazi yake.
Mtoto wa Mzee Small, Mahmood Saidi alisema kuwa baba yake alizidiwa siku ya Jumamosi asubuhi alikuwa akikohoa na kutapika damu na walimkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alisema kuwa Alifanyiwa kipimo cha CT-Scan na kubainika kuwa ana uvimbe kama wa kuvia kwa damu kichwani.