MARCIO Maximo Basilio ndiye kocha mpya wa mabingwa wa soka wa kihistoria Tanzania bara Dar Young Africans timu yenye makazi yake Kariakoo mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.
Dar Young Africans ama unaweza kuiita Yanga ni moja kati ya klabu kongwe kabisa katika bara la Afrika, Yanga ilianzishwa mwaka 1935 ikiwa klabu ya soka iliyopitia majina mbalimbali hadi kuitwa Yanga.
Unapotaja historia ya soka la Tanzania basi lazima uitaje Yanga, timu hiyo imeweza kuiletea heshima kubwa nchi hii kutokana na kandanda lake na hamasa iliyokuwa nayo kutoka kwa mashabiki wake.
Imepata kunolewa na makocha mbalimbali ambao wengine waliipa heshima klabu hiyo kwa kutwaa makombe, historia kubwa iliyonayo Yanga ni kuchukua ubingwa nje ya Tanzania, historia hiyo haijaweza kuvunjwa na klabu yoyote nchini.
Pia Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kuingia robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Yanga ilifanya hivyo mwaka 1998, lakini mafanikio ya Yanga katika soka la kimataifa bado yameonekana duni tofauti na mtani wake Simba.
Simba hasa ile ya miaka ya 70- 80 na 90 ilikuwa tishio katika soka la kimataifa baada ya kufanikiwa kuingia nusu fainali ya klabu bingwa barani Afrika mwaka 1974, Simba pia iliwahi kuingia robo fainali ya kombe la Washindi barani Afrika ambalo sasa ni kombe la shirikisho.
Mwaka 1993 ilifanikiwa kuingia fainali ya kombe la Caf na kufungwa na Stella Abijan ya Ivory Coast mabao 2-0 kwenye uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), katika mchezo wa kwanza uliofanyika huko Ivory Coast timu hizo zilitoka suluhu 0-0.
Aidha kikosi cha Simba kina historia ya kujivunia kwa kuwa ndio mabingwa wa kihistoria katika ukanda wa Afrika mashariki na kati kwa kufanikiwa kuchukua mara nyingi kombe hilo, Simba imechukua mara sita ikifuatia na AFC Leopards ya Kenya iliyochukua mara 5, Yanga ya Tanzania mara 5na Gor Mahia pia ya Kenya mara 4.
Wachezaji wa Yanga walipokuwa ziarani Uturuki
Mafanikio hayo ya Simba yalichangiwa na uongozi wake mzuri kwa kuajili makocha bora waliofanikisha kuing'arisha timu hiyo, Yanga mbali na kuwa timu ya kwanza nchini kuingia robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika, lakini haina cha kujivunia katika michuano hiyo ya Afrika.
Imekuwa mfalme katika soka la ndani na kufanikiwa kuchukua mara nyingi ubingwa wa bara, Yanga imenyakua ubingwa wa bara mara 24 huku mtani wake Simba amechukua mara 19, Yanga imekuwa mbabe zaidi kwa Simba kuanzia miaka ya 60-70 hadi 90 lakini miaka ya 2000 ufalme umehamia Simba.
Simba imekuwa na kawaida ya kumnyanyasa Yanga kila zinapokutana mpaka pale kipigo cha sharubela cha mabao 5-0 ambacho bado hakijatoka katika kumbukumbu za Wanayanga, wakati Yanga ikijitahidi kulipa kisasi, Simba inaonekana kujipanga zaidi na kukataa kurudishwa na goli hizo.
Tayari wamepata safu mpya ya uongozi ambayo ndani yao kuna wale wafuasi wa kundi la Friends of Simba ambao wana rekodi nzuri ya kuinyanyasa Yanga takribani miaka minane mfululizo ikiwa chini yake Kassim Dewji.
Wakati Simba wamejipanga, Yanga imeanza kujiimalisha zaidi ili kuhakikisha ufalme wake wa kuinyanyasa Simba pamoja na kurejea kwa kasi kwenye michuano ya kimataifa inarejea tena, uongozi wa Yanga ulio chini yake bilionea Yusuf Manji umempa mkataba aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mbrazil Marcio Maximo Basilio.
Maximo kama anavyofahamika ni kocha mwenye hamasa kubwa na amekuwa na nidhamu ya hali ya juu na mara kwa mara hataki masihara hata kidogo na wachezaji, amekuwa mstari wa mbele kuushinikiza uongozi kumpa anachokitaka na inachotaka timu.
Ameanza kwa kuutaka uongozi wa Yanga kuukarabati uwanja wake wa Kaunda ili utumike kwa mazoezi na mechi za kirafiki kwa timu hiyo, pia kukarabati hosteli zilizopo katika jengo la Yanga Jangwani.
Kocha mhamasishaji huyo ametua Yanga
Kwa kufanya hivyo Maximo anaweza kabisa kuing'arisha Yanga kimaendeleo, kikubwa anachotaka kukifanya Maximo si kuipa ubingwa wa bara peke yake, Maximo anatakiwa kuifikisha Yanga kwenye mafanikio ya michuano ya kimataifa.
Kama Yanga itaendeleza ufalme wake hapa nyumbani na kujenga heshima katika michuano ya kimataifa bila shaka Wana-Yanga watakuwa furaha kama ilivyokuwa zamani, kuna makocha wengi wamepita katika kikosi hicho siku za hivi karibuni lakini Maximo anaweza kuwa suluhisho pekee.
Watanzania tunamfahamu vema Maximo hasa alipokuwa anainoa timu ya taifa miaka minne iliyopita, Maximo ndiye kocha pekee aliyeiwezesha timu hiyo ya taifa kufuzu kwa mara ya kwanza fainali za michuano ya mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani maarufu CHAN.
Stars ilifuzu fainali hizo zilizofanyika nchini Ivory Coast mwaka 2008, tangia hapo haijafuzu tena fainali hizo na imekuwa ikiishia hatua za awali, Maximo alitoa hamasa ya kutosha na kusaidia kutengenezwa na jezi za Taifa Stars pamoja na zile za mashabiki.
Maximo ameweza kuongeza hamasa mpaka wadhamini kumiminika kuifadhili Stars, benki ya makabwela ya NMB, Bia ya Serengeti na baadaye TBL ni moja ya makampuni yaliyojitokeza kuifadhili Stars kutokana na hamasa kubwa za Maximo.
Nina imani kubwa Yanga hii ya Maximo inaweza kufikia malengo endapo tu uongozi hautamwingilia majukumu yake, najua kabisa Maximo ni kiboko ya wachezaji watoro ambao muda wote wamekuwa wakijiona miungu watu ndani ya Yanga, 0755 522216.