Uongozi wa klabu ya Yanga umetoa ruksa kwa klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini kufanya mazungumzo kama wanataka kumsajili mchezaji wao nyota, Mrisho Ngasa.
Awali klabu hiyo ilishangazwa na hatua ya klabu hiyo kubwa inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini kumchukua mchezaji wao kinyemela na kumfanyisha majaribio kinyume na taratibu na kanuni za mpira wa miguu duniani.
Ngassa alikwenda kufanya majaribio na timu hiyo ya Afrika Kusini takribani wiki mbili zilizopita, na uongozi wa timu hiyo ulikuwa tayari kutoa Sh132 milioni ili kumsajili mchezaji huyo.
Hata hivyo, mpango huo uligonga mwamba kutokana na ukweli kuwa viongozi wa Free State Stars walifanya mpango huo na Ngassa kinyemela.
Hatua hiyo iliufanya uongozi wa Yanga kulishutumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuhusika moja ka moja na mpango huo kwani haukuridhishwa na jinsi Ngassa alivyoondoka nchini kwenda Afrika Kusini wakati alikuwa kwenye Kambi ya Taifa Stars.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema kuwa wametoa fursa kwa uongozi wa timu hiyo ya Afrika Kusini kuja nchini na kufanya mazungumzo mezani ili kufanikisha suala hilo.
Njovu alisema kuwa Yanga haina haja ya kumzuia Ngassa kwenda kucheza soka lake Afrika Kusini kwani hiyo ndiyo kazi yake.
“Tutakuwa hatufanyi haki kumzuia Ngassa, lakini cha ajabu ni kwamba mpaka sasa sijamwona Ngassa kuja kuzungumzia suala hilo, nimemwona kwa mbali sana na wala hakuja kuonana na mimi, pamoja na hayo yote, sisi tupo tayari kuzungumza na timu hiyo aliyokwenda kufanya mazoezi,” alisema Njovu.
Alisema kuwa hata fedha ambazo klabu hiyo imeahidi kuzitoa kwa Yanga, wao wanazisoma kupitia mitandao tu kwani hakuna mawasiliano yoyote. “Nasisitiza waje kuonana na sisi ili kufanikisha suala hilo, hatuna kinyongo kuhusiana na mpango wake mpya, wasituogope kwani klabu yetu ipo eneo la wazi na kila mtu anaijua, ila ‘njia za panya’ hatutaki katika masuala haya makubwa yanayohusu usajili na ustawi wa wachezaji wetu,” alisema Njovu.
Ngassa alionyesha kuridhishwa na mwenendo wa suala hilo baada ya hatua hiyo ya uongozi wake.
“Sina la kuongezea, si unajua kuwa soka ni kazi yangu na masilahi ndiyo kila mtu anataka, Free State Stars wamenikubali na wapo tayari kutoa fedha kwa Yanga ili wanisajili, kinachotakiwa ni makubaliano tu kati ya Yanga na Free State Stars, sasa sijui awali ilishindikana nini,” alisema Ngassa.