come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA NAO WAIIIGA YANGA, WATUA BRAZIL KUSAKA COUTINHO WAO

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe yuko Brazil tangu juzi, mwenyewe anasema amekwenda kuangalia Kombe la Dunia, wakati tetesi zinasema amekwenda kutafuta mchezaji ili kujibu mapigo ya watani, Yanga SC.

Yanga SC imeajiri Wabrazil watatu kwa mpigo, makocha wawili, Marcio Maximo na Msaidizi, Leonardo Neiva pamoja na kiungo mshambuliaji Andrey Coutinho.


“Nimekuja kuangalia Kombe la Dunia, nashangaa hayo maneno nimefuata wachezaji yanatoka wapi, sisi hatufanyi kitu kwa sababu Yanga wamefanya, sisi tunafanya kutokana na matakwa yetu,”amesema Poppe alipozungumza jana usiku.

Poppe amesema zoezi la usajili linaendelea vizuri chini ya Makamu wake wa Kamati hiyo, Kassim Mohammed Dewji ambaye yupo nchini.

Baada ya Simba SC kupata uongozi mpya chini ya Rais Evans Aveva, haraka wamejipanga kwa ajili ya kurejesha heshima ya timu yao iliyoanza kuchakaa baada ya matokeo mabaya misimu miwili iliyopita.

Simba SC wamefanikisha usajili wa wachezaji wawili wapya hadi sasa, beki wa kushoto Mohammed Hussein Mohammed ‘Tshabalala’ kutoka Kagera Sugar na beki wa kati Joram Nason Mgeveke kutoka Lipuli ya Iringa.

Kwa sasa, Wekundu wa Msimbazi wapo katika mazungumzo na mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Paul Kiyongera ambayo yanaendelea vizuri, wakati huo huo kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Jerry Santo naye anapigiwa debe asajiliwe.

Suala la Santo linakuwa gumu kutokana na uongozi kupendekeza aende kufanyiwa majaribio, wakati kiungo huyo aliyechezea Coastal Union misimu miwili iliyopita anajiona ‘staa’ anayestahili kusajiliwa moja kwa moja.

Uongozi mpya wa Simba SC hauamini kama kuna tatizo kubwa ndani ya kikosi chao, bali matokeo mabaya msimu uliopita yalitokana na uongozi  mbovu wa wakati huo- hivyo hata usajili hautarajiwi kuwa wa kishindo sana.

Chanzo Bin Zubeiry blog