come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

WATAKAOIVAA MSUMBIJI HADHARANI


TAIFA Stars ipo vizuri kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco dhidi ya Msumbiji.

Mechi hiyo itachezea jioni ya Julai 20 mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Kocha Mkuu wa timu hiyo ya soka ya taifa ya Tanzania, Mholanzi Mart Nooij amewaambia Waandishi wa Habari leo Jijini kwamba kikosi chake kipo katika hali ya kawaida na ana matumaini ya ushindi.

Amezungumzia kambi ya Botswana iliyodumu kwa wiki mbili na kusema kwamba ilikuwa nzuri na imesaidia kuwajenga kutokana na kufanya mazoezi na kupata mechi tatu za kujipima nguvu.


Amesema katika mechi hizo, walifungwa mbili, moja dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Botswana mabao 4-2 na nyingine dhidi ya timu ya jeshi la nchini humo, BDF walishinda moja 3-1 na kufungwa moja 2-1.

Amewazungumzia wapinzani, Mambas ambao awali alifanya nao kazi akisema kwamba ni timu nzuri, anaijua na anaamini hata wao pia wanamjua. Amesema anaamini utakuwa mchezo mgumu, lakini watapambana kupata matokeo mazuri.

“Tutacheza kwa kushambulia haraka ili kutowapa nafasi wapinzani kujipanga. Naamini utakuwa mchezo mgumu, lakini hata mchezo na Zimbabwe ulikuwa mgumu na tukashinda,”amesema Nooij.

Stars ilifika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na kwenda kulazimisha sare ya 2-2 Harare.

Timu itakayofuzu hatua hii itaingia kwenye Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani.

Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kwamba maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 7,000. Amesema viingilio vingine vitatajwa baadaye.

Wambura amesema kwamba, Stars inatarajiwa kuondoka kesho kwenda Tukuyu kuweka kambi nyingine, na itarejea Dar es Salaam siku tatu kabla ya mechi.

Kuhusu wachezaji wanaocheza nje, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC na Mwinyi Kazimoto wa Al Markhiya ya Qatar, Wambura amesema TFF imekwishazitumia barua klabu zao kuwaomba kwa ajili  ya mcheo huo.

“Kama ambavyo kanuni za FIFA zinasema, wachezaji hao wanatakiwa kuwa wamefika Dar es Salaam siku tano kabla ya mechi, hivyo tunatarajia klabu hizo zitatekeleza agizo hilo,”amesema Wambura.