Ingawa sababu haswa ya Bin Kleb kujitoa haijulikani, lakini chanzo cha karibu na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, kimesema kwamba sababu za kupata muda wa kutosha kwa ajili ya biashara zake.
“Abdallah kwa muda mrefu alikuwa anaomba udhuru ili kushughulikia biashara zake ambazo zilikuwa zinakosa usimamizi wa uhakika kutokana na muda wake mwingi kufanya kazi za Yanga,”.
“Shughuli za Dar es Salaam alikuwa anazisimamia vizuri, lakini zile za nchi jirani zilikuwa zinakosa usimamizi kwa sababu muda mwingi yupo na Yanga, kabla ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu (msimu uliopita) aliomba udhuru,”.
“Na baada ya mzunguko wa kwanza pia aliomba udhuru, yote kwa sababu ya kwenda kusimamia biashara zake, sasa baada ya kuona kabisa bila kujitoa moja kwa moja, biashara zake zitayumba akamuomba Manji mapema, akiteua Kamati mpya, yeye asimuweke,”kimesema chanzo hicho.
“Manji alimkatalia mara ya kwanza, lakini ikafika wakati ikabidi amkubalie kwa sababu yeye mwenyewe Abdallah ameahidi kuendelea kuusaidia uongozi kila atakapokuwa anapata nafasi,”kimeongeza chanzo hicho.
Bin Kleb aliingia kwa pamoja na Manji, Makamu Clement Sanga na Wajumbe George Manyama na Aaron Nyanda katika uchaguzi mdogo mwaka juzi, akiwa mgombea aliyepata kura nyingi zaidi ya wengine wote.
Na katika kipindi chake, aliiwezesha Yanga kusajili wachezaji wa kiwango cha juu kama Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Emmanuel Okwi, Juma Kaseja na wengineo.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano pia, chini yake Yanga SC ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu pamoja na kuweka rekodi ya kuifunga kwa mara ya kwanza timu ya Misri, kwenye michuano ya Afrika, Al Ahly 1-0 mwaka huu.
Bin Kleb akiwa ameshika kwa pamoja Kombe la Kagame na Sanga
Seif Magari kushoto akimpongeza Bin Kleb kwa kufanikisha kumrejesha Mrisho Ngassa Yanga. Kulia kabisa ni Mussa Katabaro
Wanachama wengi wa Yanga SC bado wanaamini Bin Kleb kwa kushirikiana na ‘sahiba’ wake Ahmed Seif ‘Magari’ ndio wanaweza kupambana na Friends Of Simba ambao kwa sasa wameshika hatamu Simba SC.
Wana Yanga pia bado wanaamini kukosekana kwa Bin Kleb itakuwa pigo kwenye klabu hiyo, hususan katika sekta ya ‘fitna’ dhidi ya wapinzani wao kwenye utawala wa soka ya Tanzania kwa ujumla, Simba SC.
Jana, Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji alitangaza Kamati mpya ya Utendaji ya klabu hiyo, ambayo pamoja naye kama Mwenyekiti na Sanga Makamu wake, Wajumbe ni Abubakar Rajabu atakayesimamia pia Mradi wa Jangwani City, Sam Mapande atakayesimamia pia Sheria na Utawala Bora, George Fumbuka atakayesimamia pia Uundwaji wa Shirika, Waziri Barnabas atakayesimamia pia Vibali vya Hatimiliki na Mahusiano na Wafadhili, Abbas Tarimba atakayesimamia pia Mipango na Uratibu, Isaac Chanji na Seif Ahmed ‘Magari’ watakaosimamia pia Uendelezaji wa Mchezo, Mussa Katabalo atakayesimamia pia Mauzo ya Bidhaa, Mohammed Bhinda atakayesimamia pia Ustawishaji wa Matawi, David Ndeketela Sekione atakayesimamia pia Uongezaji wa Wanachama, Mohammed Nyenge atakayesimamia pia Utangazaji wa Habari, Taarifa na Matangazo.
Wajumbe hao, pia wataongoza Kamati ndogo ndogo, Mapande za Kamati ya Maadili, Nidhamu na Uchaguzi, Fumbuka na Barnabas Kamati ya Uchumi na Fedha Chanji na Magari Kamati za Ufundi, Mashindano naSoka la Vijana na Wanawake.
Wajumbe waliotemwa mbali na Bin Kleb ni Salum Rupia, Manyama, Nyanda na Lameck Nyambaya.