Na Mahmoud Zubeiry, BETHLEHEM
KLABU ya Free State Stars ya hapa imesema imekuwa ikimtaka sana mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco, lakini wanasikia hawawezi kumpata kwa sababu mchezaji huyo ni kipenzi cha mmoja Wakurugenzi wa timu yake Tanzania, Yussuf Bakhresa.
Meneja Mkuu wa Free State, Rantsi Mokoena ambaye ni mtoto wa mmiliki wa timu, Mike Makoena amesema kwamba wamejaribu mara kadhaa kutaka kumhamishia Bocco Afrika Kusini, lakini inashindikana.
“Bocco ni mshambuliaji wa kiwango cha kidunia, Azam inakali mafanikio yake. Kama anakuja hapa, akicheza kidogo tu mtamsikia yuko Ulaya. Ila tumekata tamaa, tunasikia yule ni kipenzi cha mtoto wa mwenye timu (Yussuf), anamlea vizuri naye ameridhika na maisha ya pale,”amesema Rantsi.
Kwa upande wake, mtoto mwingine wa mwenye timu hiyo, Kootso Mokoena ambaye ni Meneja wa timu amesema Tanzania ina wachezaji wazuri ambao amekuwa akiwaona mara kadhaa.
“Nimekuwa nikiwaona wachezaji wa Tanzania mara kadhaa, wakati fulani nilikuja Dar es Salaam mkiwa mnacheza na Msumbiji mkafungwa 1-0, kuna mchezaji nilimpenda pia, lakini nilipotaka kumchukua ikaibuka mizengwe, nikaacha,”.
John Bocco anatakiwa sana Free State ya Afrika Kusini
“Ngassa (Mrisho) nilimuona Uganda mwaka juzi (kwenye Kombe la Challenge). Nilimpenda tangu hapo, wakati wote nimekuwa nikimfuatilia bila mafanikio, na sasa tunajaribu kwa mara ya mwisho,”amesema Kootsi.
Free State Stars leo itatuma ofa ya nyongeza kidogo katika kujaribu kumnunua Ngassa, baada ya klabu yake, Yanga SC kukataa ofa ya awali ya dola za Kimarekani 80,000 zaidi ya Sh. Milioni 130, ikitaka dola 150,000 zaidi ya Sh. Milioni 240.
Ngassa tayari yuko hapa Bethlehem akifanya mazoezi na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, iliyomuajiri kocha wa zamani wa Yanga SC, Mbelgiji, Tom Saintfiet na mwenyewe ameonyesha dhamira ya kubaki.
Mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Nteze John Lungu aliwahi kuchezea Free State mwaka 1997 wakati bado inaitwa Qwa Qwa Stars kabla ya kununuliwa na familia ya Makoena mwaka 2003.
Wachezaji kadhaa wakubwa wamepitia katika klabu hiyo akiwemo Bunene Ngaduane wa DRC, Jonathan Mensah wa Ghana, Kennedy Mweene wa Zambia, John Tlale na Siphiwe Tshabalala wote wa Afrika Kusini na ambao pia wapo Bafana Bafana.