come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KWA KAULI HII, KAPOMBE ANAWAITA YANGA MEZANI

Beki mahiri wa Simba na timu ya taifa ya soka (Taifa Stars), Shomary Kapombe, amesema hamna timu ya kumng'oa kutoka Simba hapa nchini kwa sasa, na kwamba kama ataondoka Msimbazi, ataenda kutimiza ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Mkataba wa Kapombe na Simba unamalizika Aprili 12 mwakani na klabu hiyo imekuwa katika harakati za kumboreshea mkataba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kapombe, ambaye anahusishwa na mipango ya kutaka kuhamia Yanga na Azam, alisema yeye bado ni mchezaji wa Simba na anajivunia kuitumikia klabu hiyo iliyotambua kipaji chake kutoka Polisi Morogoro ambayo imeshuka tena daraja msimu huu.

Kapombe alisema kuwa ataendelea kuitumikia Simba kwa uadilifu na hatakurupuka kufanya maamuzi ya kusaini mkataba mpya baada ya huu wa sasa kumalizika.

"Mimi ni mchezaji wa Simba na naamini uwezo wangu ndiyo utanisaidia kufika mbali," alisema mchezaji huyo ambaye pia amepokea mwaliko wa kwenda kufanya majaribio Uholanzi mwezi ujao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, aliliambia gazeti hili juzi kwamba Kapombe ni mmoja wa wachezaji ambao kamati yake inajipanga kuboresha vipengele vilivyoko katika mikataba yao na vile vile ikiandaa fedha za kuwaongezea mikataba mipya.

Hanspoppe alisema kuwa Simba imejipanga kusajili wachezaji chipukizi ambao wataitumikia klabu kwa zaidi ya miaka mitatu huku ikibakisha nyota wachache wenye uzoefu.

"Kapombe ni wetu na wala hatuna wasiwasi, wanachama wasiwe na hofu kuwa anaweza kutukimbia," aliongeza.

Simba imeshaanza kuajili wachezaji baada ya kumnasa Ibrahim Twaha 'Messi' kutoka Coastal Union ya jijini Tanga.

Simba ambayo imemaliza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ikiwa ya tatu, inajipanga kwenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yatakayofanyika kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 huko Sudan.