SIMBA iliweka dau kwa kiungo mmoja matata anaitwa Haruna Niyonzima 'Fabregas'. Akaliangaliaa weee..akawaambia hapana ongezeni. Azam waliposikia na wenyewe wakaingilia kati lakini kwa kusitasita. Wakati wote huo Yanga walikuwa pembeni wanaangalia tu mchongo unavyoenda.
Fabregas akamwambia Mnyama nipe dola 50,000 (Sh.80
milioni) na mshahara wa dola 3,000 (Sh.4.8 milioni), Simba chini ya
Mwenyekiti wao wa usajili, Zacharia Hanspope wakakomalia dola 40,000
lakini baadaye wakawa wanafikiria kufika dola 50,000 wamsainishe
mchezaji huyo, Yanga wakashtukia.
Yanga, ambao tangu awali Mwenyekiti wao wa
Usajili, Abdallah Bin Kleb alikuwa akisisitiza kuwa Fabregas haendi
popote, juzi Alhamisi jioni walimkalisha chini mchezaji huyo na kumjaza
madola wakamaliza mchezo kabla ya kumtambulisha jana Ijumaa kwa
waandishi wa habari. Simba na Azam zikabaki midomo wazi.
Mwanaspoti linajua Bin Kleb ambaye amewahi kuipiga
Simba bao kwenye usajili wa Kelvin Yondani na Mbuyu Twite msimu
uliopita, alishampa Fabregas nakala ya mkataba kitambo hata kabla ya
Simba na Azam kushtukia,lakini alikuwa hajasaini kwavile walikuwa
wakibishana dau akitaka kuongezewa mshahara na dau la usajili kufikia
dola 70,000 (Sh.112milioni) na mshahara dola 3,000 (Sh 4.8milioni). Yote
hayo katimiziwa.
Mchezaji huyo anayeondoka Dar es Salaam leo
Jumamosi kwenda kwao Kigali, Rwanda alikuwa akiifanyia jeuri Yanga
kwavile alijua Simba na Azam zingempa dau hilo.
Yanga walishtuka kwamba endapo wakimuachia
akitoweka Dar es Salaam kwenda Rwanda bila saini, Simba na Azam
zingemficha na kumsainisha.
Bin Kleb sambamba na Fabregas waliuthibitishia
umma kwamba dili limekamilika na mchezaji huyo ni mali ya Yanga.
Fabregas alisema jana Ijumaa jijini Dar es Salaam kuwa: "Nimeamua
kusaini Yanga na nitaitumikia kwa nguvu zangu zote kwa miaka miwili na
sasa akili yangu naelekeza Kombe la Kagame.
"Ni kweli Simba na Azam zilinifuata, lakini
niliamua kutuliza kichwa kwanza kabla sijaamua kufanya chochote,
naheshimu kazi yangu na ningependa Mungu anijalie hata nikimaliza
mkataba huu mpya niendelee kuichezea Yanga,"alisisitiza mchezaji huyo na
kusema kwamba alizungumza na Simba na Azam kwavile alikuwa huru kufanya
hivyo ingawa alikuwa akiisikilizia Yanga.
Hata hivyo habari ambazo Mwanaspoti ilizipata jana
Ijumaa ni kwamba kuna baadhi ya viongozi walitaka Fabregas asipewe dola
70,000 lakini Bin Kleb na Seif Magari wakashinikiza asainishwe kwavile
akienda Simba au Azam itakuwa ni fedheha kubwa.
Bin Kleb alisema: "Mimi niliwaambia huyu haendi
kokote Simba na Azam zilikuwa zinajihangaisha tu. Yamesemwa mengi lakini
sisi tulitulia na kufanya mambo kwa vitendo."
Kiongozi huyo alisema wako katika mazungumzo ya
mwisho na Hamis Kiiza raia wa Uganda pamoja na Mghana Yaw Berko na
Mnyarwanda Kabange Twite ingawa Mwanaspoti linajua kwamba watamtema
Kiiza na watamsainisha Berko.
Mwanaspoti lilishuhudia Berko akimwaga machozi
akiwa amepiga magoti kwenye ofisi moja ndani ya jengo la Yanga mtaa wa
Jangwani jana Ijumaa akisisitiza kutorudia yaliyotokea msimu uliopita na
kwamba wampe mkataba mpya afanye kazi.