come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA YAMALIZA KUSAJILI, YABARIKI KUMTOSA KIIZA

Klabu ya Yanga imesema imefunga usajili wa wachezaji wazawa, siku mbili baada ya kumchukua mlinda mlango Deogratias Munishi 'Dida' kutoka timu ya Azam.

Akizungumza  jana, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga Abdallah bin Kleb alisema wamefanyia kazi mapendekezo ya kocha Ernest Brandts juu ya wachezaji wazawa aliokuwa akitaka kuwaongeza kwenye kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Bin Kleb alisema usajili wa mlinda mlango huyo ambaye amewahi kuzichezea Simba kabla ya kuhamia Azam, ulipendekezwa na Brandts baada ya kuachana na mpango wa kumsajili kipa wa zamani Mghana, Yaw Berko.

"Usajili wetu umefanyika baada ya mapendekezo ya kocha wetu... ni yeye aliyetaka tumsajili Dida na tumefanya hivyo," alisema Bin Kleb.

Aidha, alisema baada ya Dida hakuna nafasi ya mchezaji wa ndani kwa kuwa tayari wamemaliza kufanyia kazi mapendekezo ya Brandts kwa upande wa wazawa.
Alisema wataongeza mchezaji mwingine mmoja kutoka nje ya nchi bila ya kumtaja mchezaji huyo wala nchi anayotokea.

"Siwezi kukuambia kitu ambacho hatujakikamilisha," alisema Bin Kleb ambaye kamati yake ilifanya usajili mzuri ulioongeza rekodi kwa kuipa ubingwa wa 23 wa Bara msimu uliopita na kuelekea kurudia jambo hilo tena katika dirisha hili.

"Tupo kwenye mazungumzo na mchezaji wa nje ya nchi na mambo yakiwa tayari tutaweka wazi kama ilivyokawaida yetu."

Hata hivyo, taarifa zilizozagaa ni kuwa Yanga ipo kwenye mbio za kumsajili mshambuliaji wa Uganda anayewaniwa pia na Simba, Moses Oloya anayecheza soka nchini Vietnam.

Yanga inaendelea kusajili mchezaji wa ziada wa kigeni baada ya shirikisho la soka, TFF, kuahirisha hadi msimu ujao kuanza kutumika kipengele cha Azimio la Bagamoyo la mwaka 2010 ambacho kinataka timu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni.

Yanga imeshawasajili Haruna Niyonzima (Rwanda), Didier Kavumbagu (Burundi) na Mbuyu Twite (JK Kongo) kutoka nje ya nchi mpaka sasa.