KATIKA kuhakikisha inaanza vema Ligi Kuu Bara, timu ya Ashanti United (Pichani) ya Ilala jijini Dar es Salaam, ipo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kupiga kambi nchini Burundi.
Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, itafungua pazia la ligi hiyo kwa kucheza na mabingwa watetezi, Yanga katika mechi itakayopigwa Agosti 24, mwaka huu Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Abubakar Silas, alisema, wanakamilisha taratibu za safari hiyo na itakapokamilika watatangaza siku ya kuondoka.
"Kama mnavyojua, tumepanda daraja na lengo letu si kuwa wasindikizaji, ila kuwa timu ya ushindani, hivyo tunajipanga kuleta mageuzi katika soka letu na tutakwenda Burundi kupiga kambi," alisema Silas.
Alisema, kabla ya kwenda huko, watakwenda mkoani Kigoma kupiga kambi ya muda, ambako baadaye watakwenda nchini humo.
Alisema, kambi hizo zitachukua mwezi mzima, ambako wakija jijini Dar es Salaam, moja kwa moja ni kuwavaa Yanga.
Aliongeza kuwa, wakiwa nchini Burundi, watacheza mechi mbili au tatu za kirafiki na kwamba, mawasiliano yanakwenda vizuri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na Chama cha Soka Burundi ili kufanikisha safari hiyo.