
Kikosi cha Azam FC
Akizungumza na mtandao huu jijini Dar es Salaam jana, katibu mkuu wa klabu hiyo, Idrissa Nassoro, alisema kikosi chao kinachonolewa na kocha Muingereza Stewart Hall kitaondoka nchini baada ya mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) ya timu ya taifa (Taifa Stars) dhidi ya Uganda itayopigwa Julai 29 jijini Kampala, Uganda.
Taifa Stars, itakayoingia kambini keshokutwa, itacheza mechi ya kwanza dhidi ya The Cranes Julai 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
"Tulitaka timu yetu iweke kambi Afrika Kusini kwa muda mrefu zaidi lakini ratiba ya Taifa Stars ndiyo inatulazimisha kusubiri mpaka mechi ya marudiano ya mechi dhidi ya Uganda," alisema Nassoro.
"Timu yetu ambayo iko kambini Dar es Salaam itakamilika kesho (leo) baada ya kurejea kwa wachezaji waliokuwa na timu zao za taifa. Jumatano tutalazimika kuwakosa wachezaji wetu kadhaa ambao watajiunga na kambi ya Stars."
Alisema kikiwa Afrika Kusini, kijkosi chao kitapata nafasi ya kujipima na timu mbalimbali nchini humo na kurejea siku chache kabla ya mechi yao ya kuwania Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga itakayochezwa Agosti 17.
Kwa nyakati, Azam waliomaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya Bara waliweka kambi Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako walishiriki mashindano ya hisani na kutwaa ubingwa.