come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

BAKHRESSA ATAPELIWA ZANZIBAR, TIMU ALIYOINUNUA ILIUZWA KWA MALINDI

HATUA ya kuuzwa kwa daraja la ligi kuu la timu ya Bandari SC, imeibua utata baada ya kubainika kuwa kuna barua mbili zinazoelezea kuuziwa timu mbili tafauti.
 

Barua hizo ni pamoja na ile iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa timu hiyo Julai 1, 2013 kwenda Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ikitoa taarifa kwamba muafaka umefikiwa kwa daraja hilo kuuziwa timu ya Azam FC ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye nambari ya kumbukumbu ZPC/BSC/VOL1/40/2013, muafaka huo umepatikana katika mkutano wa wanachama, viongozi na wachezaji wa timu hiyo ambapo wanachama 71 walitia saini waraka kuunga mkono uamuzi huo.
Uamuzi wa kulitema daraja la timu hiyo umechukuliwa baada ya Shirika la Bandari Zanzibar kujivua jukumu la kuiendesha timu kwa kile kilichoelezwa kukimbia gharama.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, Katibu wa Azam Nassor Idrissa Mohammed na mwenzake wa Bandari SC Makame Silima Makame, wote walikiri kukutana na kukubaliana kuuza na kununua nafasi hiyo.
Hata hivyo, Idrissa alisema baada ya maafikiano hayo, Azam FC imeliachia suala,hilo kwa wanasheria wake ili kuangalia sheria na kanuni za ZFA zinavyoelekeza kabla ya kumalizana na wavuta nanga hao.
Katibu Mkuu wa ZFA Kassim Haji Salum alikiri kupokea barua ya Bandari iliyosainiwa na Katibu wake ambaye, alidai chama hicho ndiye kinayemtambua.
Hata hivyo, siku chache baada ya taarifa hiyo, Zanzibar Leo ilifanikiwa kupata nakala ya barua nyengine iliyoandikwa na kutiwa saini na Hamza Mohammed Ali kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, inayothibitisha kuwa daraja la timu hiyo limeuzwa kwa timu ya Malindi SC. 
Aidha barua hiyo ya Juni 27, 2013 yenye nambari ya kumbukumbu ZPC/M/75 imeambatana na nakala ya risiti nambari 2760 inayoonesha kuwa Malindi imelilipa shirika hilo shilingi milioni tano taslim, ikiwa gharama za kununua nafasi ya Bandari SC katika ligi kuu msimu ujao.
“Uongozi wa shirika umekubali ombi lenu la kupatiwa daraja la timu ya Shirika la Bandari ya mpira wa miguu, kwa vile haitashiriki kwenye ligi ya daraja linalohusika kwa msimu wa 2013/2014”, ilisema sehemu ya barua hiyo, ambayo hata hivyo, nakala yake haikutumwa ZFA
“Uamuzi huo wa nyinyi kupatiwa daraja hilo utatekelezwa kwa malipo ya TShs, 5,000,000 na kulipwa kabla ya makabidhiano”, iliongeza barua hiyo.
Aidha, uongozi wa Shirika la Bandari ulisema kuwa, hatua na taratibu zote za kisheria pamoja na gharama nyengine ambazo zitajitokeza katika kukamilisha suala hilo, litakuwa ni juu ya mnunuzi huyo, timu ya Malindi.
Kutokana na hali hiyo, kuna fununu kwamba uongozi wa Malindi SC unakusudia kuifikisha kadhia hiyo katika vyombo vya sheria ili kupata suluhisho.
Nao uongozi wa ZFA umeshikilia msimamo wake wa kuitambaua hatua ya kuuzwa daraja hilo kwa matajiri wa ngano na vyombo vya usafiri wa baharini, Azam FC, kwa madai kuwa, mwanachama wao ni Katibu wa timu na si Mkurugenzi wa shirika.