PACHA wa muigizaji wa filamu nchini na mwanamuziki, Husna Posh ‘Dotnata’, Dometria Alphonce ‘DD’, anatarajia kuikamata Mbeya Agosti 4 atakapotua katika ukumbi wa kanisa la Makimbilio kuhudhuria tamasha kubwa la muziki wa Injili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa tamasha hilo, George Kayala, alisema kuwa pacha huyo ambaye anashughulikia kuitoa filamu yake mpya iitwayo ‘Kua Uyaone’ inayosimulia mkasa wa kweli uliowahi kumpata katika maisha yake ya ndoa, ataambatana na wakali wengine wa filamu kutoka jijini.
“Msanii huyu wa filamu amekubali kufika katika tamasha kubwa la muziki wa Injili na atakwenda na wasanii wenzake kutoka jijini Dar es Salaam, ambao watakwenda kumuunga mkono Mwinjilisti Kabula katika kuitambulisha albamu yake mkoani Mbeya,” alisema Kayala.
Kayala alisema kuwa lengo la kufanya tamasha hilo ni kukusanya fedha za kununua vyombo vya muziki, ambavyo vitamsaidia Kabula kulihubiri neno la Mungu ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
“Tamasha hilo tumeandaa kwa ajili ya kuitambulisha albamu ya ‘Nitang’ara Tu’ katika mkoa wa Mbeya na kwa mara ya kwanza itauzwa kwa wakazi wa mkoa huo ambao wamekuwa wakiiomba kwa muda mrefu,” alisema Kayala.
Kayala, alitaja kiingilio katika tamasha hilo kuwa ni sh 2,000 kwa mtu mzima na 1,000 kwa mtoto na shughuli itaanza saa 7:00 mchana na kumalizika majira ya saa 12:00 jioni.
Pacha huyo wa Dotnata, alikiri kupata mwaliko huo na kusema kuwa atakwenda Mbeya kuwahamasisha wamuunge mkono Kabula, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaisukuma mbele kazi ya Mungu.
“Nikweli nitakuwepo katika tamasha kubwa la muziki wa Injili ambalo litafanyika katika ukumbi wa kanisa la Makimbilio mkoani humo na nitaambatana na wasanii wengine wakali wa filamu, ambao nitawaweka hadharani siku si nyingi,” alisema pacha huyo wa Dotnata.
Amewataka wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake, kufika kwa wingi katika tamasha hilo ambalo limeandaliwa na GMK Production kwa ajili ya kuitambulisha albamu ya tatu ya mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Mwinjilisti Kabula George.
Tamasha hilo linadhaminiwa na Ushindi Redio FM ya Mbeya, RGC Miracle Center Tabata Chang’ombe, Shalom Production, DD Entertainment, The Genesis Global College na Eck Production.
