Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliofanyika jana (Julai 13 mwaka huu) umepitisha marekebisho ya Katiba yake, hivyo mchakato wa uchaguzi unatarajia kuanza wakati wowote.
Wajumbe
zaidi ya 100 walihudhuria Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa NSSF
Waterfron, Dar es Salaam na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Joel Bendera aliyewataka wajumbe kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu
nchini kinakuwa.
Mkutano
huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga umefanya
marekebisho ya Katiba kutokana na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA). James Johnson kutoka Idara ya Wanachama ndiye
aliyeiwakilisha FIFA katika mkutano huo.
Aprili
mwaka huu FIFA ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza
kwanza yafanyike marekebisho ya Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili,
na Kamati ya Rufani ya Maadili ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo
ya kimaadili kwa familia ya mpira wa miguu nchini.
Mbali
ya kamati hizo, mabadiliko hayo pia yametengeneza ngazi mbili za
kushughulikia masuala ya kinidhamu ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na
Kamati ya Rufani ya Nidhamu.
Kamati
ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Tenga itakutana kesho (Julai 14 mwaka
huu) kwa ajili ya kuteua wajumbe watakaounda Kamati hizo ili kuruhusu
kuanza mchakato wa uchaguzi ambao FIFA iliusimamisha hadi vitakapoundwa
vyombo hivyo.