come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA RAHA TUPU-BRANDTS

KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts, amesema uwepo wa nyota wote katika mazoezi kwa sasa kunafanya programu zake ziende sawa, huku akionya kuwa atakayebweteka asitarajie kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.


Akizungumza jana, Brandts alisema awali programu zake zilikuwa haziendi vizuri kutokana na baadhi ya wachezaji kuwamo katika kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.

Brandts alisema anapata faraja kwa vile nyota wote wanafika kwenye mazoezi, hivyo ni imani yake timu yake itafanya vema katika mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Ashanti United, akitoka kucheza na Azam FC Agosti 17 katika mechi ya Ngao ya Jamii.

Aidha, Brandts alisema pia anafurahia ujio wa Mrisho Ngasa aliyejiunga nayo akitokea Simba alikocheza msimu uliopita baada ya kuondoka Jangwani msimu wa 2009/10 kwenda Azam kwa kitita cha sh mil. 58.

“Sasa timu yangu iko sawa. Na itaendelea kuwa sawa kutokana na wachezaji wote kuripoti mazoezini na ujio wa Ngasa utasaidia, kwani ni mchezaji niliyewahi kumwona akicheza kwa kasi kiasi cha kuwapa tabu mabeki,” alisema Brandts.

Kuhusu wachezaji, Brandts amewataka kutobweteka kwani hakuna aliyejihakikishia kikosi cha kwanza, akisema kupangwa kwa mchezji kutategemea uwezo na kujituma kwenye mazoezi.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo umeshindwa kufanyia kazi ombi la kocha la kuweka kambi nje ya nchi na kutakiwa kubaki jijini kujiandaa na mechi ya Ngao ya Hisani Agosti 17.

“Kocha alipendekeza kambi nje ya nchi, lakini majukumu yamekuwa mengi na fedha nyingi tumetumia kwenye usajili, hivyo hakutakwenda nje kupiga kambi,” kilisema chanzo kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo jana.