AZAM
FC jana ilianza vyema kampeni zake za kuwania ubingwa wa Kombe la
Shirikisho Afrika baada ya kuifunga klabu ya Ferroviario de Beira ya
Msumbiji kwa goli 1-0 katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya kwanza ya
raundi ya awali kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.Kipre Tchetche alifunga goli la kwanza kwa Azam baada ya kupata pasi ya Brian Umony na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Ferroviario, Willard Manyatera na kutinga wavuni katika dakika ya 41.
Wenyeji Azam walianza vyema mechi hiyo kwa kulishambulia lango la Ferroviario tangu mapema. Khamis Mcha alikuwa katika nafasi ya kufunga katika dakika ya nne tu ya mchezo lakini shuti lake liliokolewa na beki Reinildo Mandava.
Dakika moja tu baadaye wageni walijibu mapigo kupitia kwa nahodha wao Manuel Fernandes lakini shuti lake lilidakwa kiufundi na kipa wa Azam, Mwadini Ali.
Mario Sinamunda wa Ferreviario alipata mwanya katika dakika ya 10 lakini shuti lake lilidakwa na kipa Mwadini.
Kipa wa Ferroviario, Manyatera alidaka shuti la Kipre kufuatia pasi ya Mcha katika dakika ya 12 na dakika sita baadaye Kipre alidondoka ndani ya boksi na kuifanya pasi 'tamu' ya Himid Mao kupotea na kumpa nafasi beki wa wageni, Zefanias Matsinhe kuokoa hatari hiyo langoni mwao.
Umony alikaribia kuifungia Azam bao la pili katika dakika ya pili baada ya mapumziko wakati alipowachambua mabeki wa Ferreviario na kubaki na kipa lakini akapiga shuti juu ya lango na kupoteza nafasi ya wazi.
Himid
Mao alipoteza nafasi nyingine ya kufunga katika dakika ya 73 wakati
kichwa chake kiliposhindwa kulenga lango kufuatia krosi ya Malika Ndeule
katika dakika ya 83.Kocha Hans der Pluijm wa Yanga, ambao juzi walishinda 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro katika mechi yao ya hatua ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, akiwa na baadhi ya nyota wa mabingwa hao wa Tanzania Bara kama Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza na Juma Kaseja walikuwapo uwanjani Azam Complex kuwashuhudia vinara hao wa ligi Azam.
Azam FC: Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Said Morad, Michael Bolou, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Himid Mao, Khamis Mcha/ Johh Bocco 'Adebayor' (dk. 61), Kipre Tchetche na Brian Umony/ Jabir Aziz (dk.71).
Ferroviario: Willard Manyatera, Zefanias Matsinhe, Emidio Matsinhe, Abrao Cufa/ Kiki Simao (dk.77), Edson Morais, Reinildo Mandava, Valter Mandava/ Henry Antony (dk.46), Antonio Machava, Manuel Fernandes, Mario Sinamunda, Manuel Coreeia/ Djei Buzana (dk.71).