come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MBEYA CITY YATISHIA KIBARUA CHA LOGA SIMBA

Zikiwa zimesalia siku mbili kabla kuvaana na wapinzani wao Mbeya City, Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic ameingia hofu ya pambano hilo litakalopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Timu hiyo itajitupa uwanjani kuvaana na Mbeya City ikiwa imetoka kwenye maumivu ya kuchezea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya JKT Mgambo, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kutoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar mkoani Morogoro.

Simba yenye pointi 31 inahitaji ushindi wa aina yoyote ile ili ijiwekee mazingira mazuri ya ubingwa unaowaniwa na Azam FC wenye pointi 36, Yanga 35 na Mbeya City 34.


Logarusic alisema kuwa anatarajia kuvaana na moja ya timu ngumu na yenye  ushindani inayowania ubingwa katika msimu huu, hivyo hatarajii kupata wepesi katika mechi hiyo kutokana na ubora wa kikosi chao.

Logarusic alisema, Mbeya City inaundwa na wachezaji wengi chipukizi wenye kazi na morali ya hali ya juu na wanaocheza kitimu, hivyo anaendelea kukinoa kikosi chake kwa kuangalia sehemu zenye upungufu kwa ajili ya kuziimarisha kabla ya kuwavaa wapinzani wake.

“Mechi ya Mbeya City ni ngumu kutokana na ubora wa timu yao inayocheza pamoja na kujituma kwa  kila mmoja kutimiza majukumu yake ndani ya uwanja, hivyo tuna kibarua kigumu katika kupata ushindi kwenye mechi hiyo.

“Siyo timu nyepesi ya kuidharau hakuna mtu asiyeijua, ni kati ya timu inayowania ubingwa huu wa ligi pamoja na klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC, nitajitahidi kuimarisha kikosi changu ili tuhakikishe tunapata matokeo mazuri katika mechi hiyo.”