come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MGAMBO YAIADHIRI SIMBA, YAIPIGA 1-0 MKWAKWANI

Simba ilipoteza nafasi ya kusogea zaidi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakati ilipokubali kipigo cha goli 1-0 kutoka kwa timu iliyokuwa ikishika mkia ya Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga jana.

Kilikuwa ni kisasi kizuri kwa Mgambo ambayo katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza msimu huu ilisambaratishwa kwa magoli 6-0 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi huku mshambuliaji Amisi Tambwe akiweka rekodi mpya ya 'hat-trick' iliyomshuhudia akifunga magoli manne jioni hiyo.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kuanguka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 31, tatu nyuma ya Mbeya City iliyopanda hadi nafasi ya tatu kwenye ligi baada ya jana kuifunga Mtibwa Sugar 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.


Simba iliyoshuka uwanjani mara 17, imecheza mechi moja zaidi ya Azam iliyo kileleni na pointi 36 na Yanga iliyo katika nafasi ya pili kwa pointi 35. Yanga na Azam hazikucheza mechi zake za ligi wikiendi hii kutokana na kuwa na jukumu la kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa jana na juzi.

Kilikuwa ni kipigo cha kwanza kwenye ligi kwa kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic, kilichomaanisha kwamba kocha huyo mwenye makeke ameambulia pointi moja katika mechi mbili zilizopita baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar katikati ya wiki iliyopita.

Simba itakuwa na mtihani mkubwa katika mechi yake ijayo wakati itakapoikabili Mbeya City ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi hii.

Maganga Fully aliipatia Mgambo goli la kuongoza lililodumu hadi mwisho wa mchezo katika dakika ya 25 akiunganisha mpira uliookolewa na Ivo Mapunda kufuatia shuti la mpira wa 'fri-kiki'.

Wakati timu zikienda mapumziko Mgambo walikuwa mbele kwa goli 1-0 huku wenyeji wakitawala mchezo hasa eneo la kiungo ambalo nyota wa Simba kama Jonas Mkude, Amri Kiemba na Awadhi Juma walipoteana.

Kipindi cha pili, Simba walicheza vizuri zaidi wakielewana na kulishambulia mfululizo lango la Mgambo lakini wenyeji walisimama kidete kuhakikisha wanalipa kisasi.

Kwenye Uwanja wa Sokoine, Mtibwa Sugar walitangulia kupata goli kupitia kwa Jamal Mnyate katika dakika ya 53, lakini wenyeji Mbeya City walicharuka na kusawazisha goli hilo dakika nne tu baadaye kupitia kwa Peter Mapunda kabla ya Hamad Kibopile kufunga la ushindi katika dakika ya 67.

Haruna Moshi 'Boban' alifunga goli la pekee lililoipa Coastal Union ya Tanga ushindi wa goli 1-0 ugenini dhidi ya Rhino Rangers. Alifunga goli hilo mapema katika dakika ya 8 tu ya mchezo lililoifanya Coastal kufikisha pointi 22 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya sita ikiishusha Kagera Sugar ambayo nayo jana ilifikisha pointi 22 baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Oljoro JKT mjini Arusha.

Kagera Sugar ilitangulia kupata goli katika dakika ya 7 kupitia kwa Themi Felix kabla ya wenyeji kusawazisha katika dakika ya 82 kupitia kwa Jacob Masawe.

Yanga na Azam hazitacheza mechi yao ya mkononi hadi Februari 26 kutokana na kutumia muda huu kujiandaa na mechi zao za marudiano za kimataifa. Katika mechi hizo Yanga itaivaa Prisons jijini Dar es Salaam na Azam itacheza dhidi ya Ashanti.

Simba: Ivo Mapunda, Haruna Shamte/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk.57), Issa Rashid 'Baba Ubaya', Donaldo Mosoti, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Awadhi Juma, Amisi Tambwe, Ali Badru/ Haruna Chanongo (dk.57), Ramadhani Singano 'Messi'.

Mgambo: Saleh Tendega, Bashir Chanache, Salim Kipaga, Bakar Mtama, Novarty Lufunga, Mohamed Samata, Peter Mwalyanzi, Bolly Ajalli, Maganga Fully na Malimu Busungu.