TIMU
ya Tabata Veterans, imeandaa bonanza maalum la kumuenzi aliyekuwa
mchezaji wa timu hiyo, Omary Changa aliyefariki dunia mwezi uliopita,
ambalo litafanyika Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Tabata Shule, Dar
es Salaam.
Mwenyekiti
wa Tabata Veterans, Rodgers Peter ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii
kwamba maandalizi yote ya bonanza hilo la kutathmini mchango wa mwenzao
huyo aliyetangulia mbele ya haki yamekwishakamilika.
“Maandalizi
yamekamilika na tunatarajia litakuwa bonanza zuri na sehemu nzuri ya
watu kukutana na kukumbuka kuhusu Omary Changa, ambaye alikuwa mtu wa
watu kwa kweli,”alisema Peter.
Peter
alisema bonanza hilo litakaloanza saa 2:30 asubuhi, litahusu michezo
mbalimbali ikiwemo soka na litafuatiwa na burudani nyingine baadaye
kabla ya kufungwa Saa 12:00 jioni.
Peter
amewaomba wadau na wapenzi wa soka Tabata kujitokeza kwa wingi siku
hiyo ili kuungana na wenzao kumuenzi marehemu Changa, ambaye enzi zake
alichezea Yanga SC, Moro United na Kagera Sugar ya Bukoba.