Yanga leo inashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na Ruvu Shooting huku
kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Van der Pluijm akipanga kumtumia
mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa mara ya kwanza kwenye michezo ya ligi kuu
ya Bara.
Okwi hajaichezea timu hiyo mchezo wowote wa ligi tangu
alipotua timu hiyo katika dirisha dogo la Januari kutokana na utata
uliokuwapo kwenye usajili wake.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto, alisema Pluijm anaweza akamtumia Okwi leo kulingana na mahitaji yake.
"Suala
la Okwi kucheza au kutocheza hilo lipo mikononi mwa kocha kulingana na
kikosi chake atakachokipanga kesho," alisema Kizuguto kwa sababu "kocha
kwa sasa yupo huru kumtumia na kutokana na mazoezi ya leo (jana) asubuhi
ni wazi atamtumia."
Aidha, Kizuguto alisema Pluijm anajivunia ushirikiano na umoja wa wachezaji wake wanaoendelea kuuonyesha klabuni hapo.
Mashabiki
wa klabu hiyo wana hamu kubwa ya kumuona kwenye ligi mshambuliaji
Mganda huyo ambaye alifanya vizuri akiwa na klabu yake ya zamani ya
Simba hapa nchini kabla ya kuuzwa kwa klabu ya Etoel du Sahel ya Tunisia
miezi 13 iliyopita.
Yanga inavaana na Ruvu Shooting ikitokea
kwenye mashindano ya kimataifa ambapo iliitoa Komorozine ya Comoro kwa
jumla ya magoli 12-2 kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa
Afrika.
Van Pluijm alisema michezo ya ligi kuu ni sehemu ya
maandalizi kabla ya kuvaana na mabingwa watetezi Al-Ahly ya Misri
Jumamosi ijayo katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya
Afrika.
Mbali na kutumia ligi kuu ya Bara kama mazoezi ya
maandalizi, timu hiyo ilimtuma kocha msaidizi Charles Mkwasa Misri
kushuhudia mchezo wa Super Cup kati ya Alhy na mabingwa wa Kombe la
Shirikisho la klabu za Afrika CS Sfaxien ya Tunisia.
Mkwasa aliyerejea jana, alitumwa kuwasoma mabingwa mara nane hao Afrika kabla ya kuvaana nao Machi mosi.