STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi aliwaambia Yanga wasije uwanjani siku ya mechi ya watani wa jadi lakini kiungo Mbrazili, Andrey Coutinho amejibu mapigo
Coutinho raia wa Brazil alisema ameishuhudia Simba ikicheza mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya Coastal Union na kugundua kuwa Yanga ina jeuri kubwa ya kushinda Oktoba 18.
Coutinho alisema ameiangalia safu yao ya ushambuliaji na kuilinganisha na ile ya ulinzi ya Simba na kupata jibu kwamba wanakila sababu ya kupata ushindi ambapo sasa anataka kutumia mchezo ujao dhidi ya JKT Ruvu kujiweka sawa kabla ya kukutana na Mnyama.
“Nitakuwa sawa zaidi baada ya mchezo ujao dhidi ya JKT Ruvu, hatuna sababu ya kukosa ushindi dhidi ya Simba, nimewaona tuna nguvu kubwa ya kupata ushindi, tunawaheshimu Simba wana timu nzuri lakini kwangu naona Yanga tunazidi katika ubora, nitafurahi nikicheza katika mchezo huo sasa najipanga kuhakikisha nikipata nafasi katika mechi hiyo nifanye nini nikishirikiana na wenzangu nataka niisaidie Yanga kushinda mechi muhimu kama hiyo.”
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo anapiga hesabu ili kuona Genilson Jaja anafunga zaidi baada ya kugundua Mbrazili huyo anavyochungwa na mabeki watatu asifunge.
Maximo alisema katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons Jaja alikuwa akikabwa na mabeki watatu ambapo sasa anamuandaa mshambuliaji Mrisho Ngassa kumpunguzia ulinzi Mbrazili huyo.
“Jaja alikuwa anachungwa na mabeki watatu ni vigumu kufunga hapo lakini hilo ni tatizo linalosababishwa na Ngassa kucheza mbali na Jaja, Ngassa ni lazima awe karibu na Jaja kupunguza nguvu na mabeki kumchunga Jaja najua kinachotakiwa kufanyika sasa nafikiri kutakuwa na mabadiliko katika mechi zijazo.”