Kocha wa Simba, Patrick Phiri, amesema kuwa matokeo ya sare ya mabao 2-2 ambayo timu yake ilipata katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga yalisababishwa na sehemu ya kiungo 'kufa'.
Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Phiri alisema kuwa baada ya Haroun Chanongo, kuumia na kutoka, katika kipindi cha pili, kikosi chake kilielemewa.
Phiri alisema kuwa hali hiyo iliruhusu wapinzani wao kutawala eneo hilo na hatimaye walisawazisha mabao yote mawili wakitokea nyuma.
Mzambia huyo alisema pia Coastal ina wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao waliwapa "shughuli nzito" hata pale Simba ilipokuwa inaongoza kwa mabao 2-0.
Alisema pia Ligi Kuu ni ngumu na mara nyingi mechi za kwanza huwa ngumu na hutoa matokeo ya kushangaza kwa baadhi ya timu.
"Kiungo ndiyo kiliifanya timu yetu ipoteze mwelekeo. Hasa kipindi cha pili hakikuwa kizuri kwetu," alisema Phiri ambaye amerithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Alisema kuwa leo timu yake inaendelea mazoezi kwa ajili ya mechi yao ya pili dhidi ya Polisi Morogoro itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi.
Naye nahodha wa Simba, Joseph Owino alisema kuwa matokeo hayo yamewasikitisha kutokana na wao kuonyesha uwezo wa juu ukilinganisha na Coastal Union.
Owino alisema kuwa wanajipanga kurekebisha makosa yaliyotokea ili wapate ushindi katika mechi inayofuata.
Ndanda kutoka Mtwara ndiyo timu inayoongoza katika msimamo wa ligi baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya wageni wenzao katika ligi timu ya Stand United ya Shinyanga.