come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SUMAYE AUPONDA UTAWALA WA MKAPA KWA KUUA MICHEZO MASHULENI

Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema uongozi wao ulikosea kimsingi kufuta michezo shuleni.

Mwishoni mwa 1996, Serikali kupitia aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya michezo, Joseph Mungai ilipiga marufuku michezo yote kwenye shule za umma.


Katika tangazo lake, Mungai ambaye alikuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), alisema uamuzi huo ulichukuliwa ili kuepusha muda mwingi wa masomo uliokuwa ukipotea kwa wanafunzi kushiriki michezo.

Mungai alieleza wakati ule kuwa wanafunzi nchini walihitaji muda wa saa 198 kwa ajili ya masomo kwa mwaka, lakini nyingi kati ya hizo zilipotea bure kwenye shughuli nyingine, zikiwamo michezo.

Lakini, akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalumu nyumbani kwake, Kiluvya, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, Sumaye aliukosoa uamuzi huo.

“Lazima nikiri kuwa ‘tuli-overreact’ (tulitoa uamuzi mkubwa mno) kufuta michezo katika shule zetu,” alisema Sumaye, ambaye anajianisha mwenyewe kuwa mwanamichezo.

Alisema yeye ni mpenzi wa timu yoyote inayofanya vyema katika michezo, ingawa binafsi amekuwa akifahamika kuwa shabiki wa Simba.

Aliongeza kuwa ingefaa michezo iendelee katika shule zote, ila kwa kuzingatia uwiano wa muda ambao unatumika katika kutoa taaluma na kucheza na kuongeza kuwa michezo inaweza kuisaidia Tanzania kujitangaza.

“Kimsingi, tulitakiwa tufahamu kuwa michezo pia ina umuhimu wake kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu, wala si kuiondoa kijumla,” alisema.

Aliongeza: “Tungeangalia aina ya michezo kwani inao umuhimu kwa maendeleo ya nchi, hata kujenga afya, miili na akili za vijana wetu.”

Alisema walisikia malalamiko ya baadhi ya wazazi, walezi kwamba vijana wao walikuwa wakipoteza muda kushiriki michezo tangu ngazi ya elimu ya msingi, sekondari hadi vyuo, jambo ambalo lilisababisha michezo yote kufutwa katika mtalaa wa masomo.

Alisema makosa hayo bado yanamsumbua hadi leo, ingawa anajivunia ujenzi wa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000.