Mrembo kutoka Temeke Sitti, Mtemvu ametwaa taji la Reds Miss Tanzania 2014 katika mashindano yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Ushindi wa Sitti umezua mjadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii pamoja na mashabiki waliohudhuria mashindano hayo kuonyesha wazi wasiwasi wao kuwa mrembo huyo ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu hakustahili kushinda kwani alitoka nje ya mstari katika kujibu swali linalohusu uzazi wa mpango.
Katika kujibu swali hilo ambalo lilikuwa la kuchagua lugha kati ya Kiswahili na Kingereza, Sitti alichagua Kingereza, lakini aliwaacha watu midomo wazi kwani alitumia lugha ya Kifaransa.
Kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Sitti alikuwa na mashabiki wengi ambao walitoka Temeke wakiwa na mabango ya kumnadi kuwa ndiye Miss Tanzania.
“Katika majaji ni nani anayejua lugha ya Kifaransa alichokijibu wanakielewa, tulijua tangu mwanzo yeye ndiye atapewa, maana hata kwenye Televisheni za ukumbini anaitwa mwingine picha inayoonyeshwa ya kwake,” alisikika mmoja wa mashabiki baada ya Sitti kutangazwa mshindi.
Hata hivyo, Mratibu wa mashindano hayo, Hashimu Lundenga alisema, “Wasichana wengi ni wazuri, kila mmoja alistahili kushinda na maneno kama hayo ya upendeleo tumeshayazoea hakuna mwaka ambao mshindi katangazwa yakakosekana maneno.”
Katika mashindano hayo mshindi wa pili alikuwa Lilian Kamazima, wa tatu ni Jihan Dimachk, nafasi ya nne ilienda kwa Dorrice Mollel huku Nasreen Abdul akichukua nafasi ya tano.
Taji la Photogenic lilinyakuliwa na Evelyne Baasa, vipaji maalumu lilienda kwa Nicole Sarakikya, taji la Personality limetwaliwa na Salama Salim, huku lile la Top Model likichukuliwa na Jihan Dimachk.