Magoli kutoka kwa beki Kelvin Yondani na kiungo Haruna Niyonzima yalitosha kuipa Yanga ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibwaga JKT Ruvu kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, walikuwa ni Mtibwa Sugar waliokaa kileleni kwenye msimamo baada ya kupata ushindi wa tatu mfululizo jana wakiifunga Mgambo kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani kupitia bao la Ally Shomari.
Matokeo hayo yalimaanisha kwamba mabingwa Azam wako katika nafasi ya pili wakiwa na pointi saba baada ya juzi kushikiliwa kwa sare ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Yanga iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita.
Beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani aliifungia timu yake goli kwa shuti kali lililompita ubavuni kipa Jackson Chove wa JKT dakika ya 36.
Mfungaji aliitendea haki pasi murua ya nje ya boksi ya kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas' aliyerejea katika makali yake baada ya kufanya vibaya msimu uliopita kutokana na maradhi.
Hadi mapumziko, wenyeji walikuwa mbele kwa goli 1-0.
Mshambuliaji Idd Mbaga alikuwa tishio kwenye lango la Yanga kipindi cha kwanza akipiga mashuti matatu makali likiwamo la dakika ya 15 lililogonga mwamba na kuzaa kona baada ya kipa Deogratius Munishi 'Dida' kuugusa kwa vidole mpira wa kombora hilo.
Niyonzima aliifungia Yanga goli la pili kwa mpira wa adhabu uliotengwa nje kidogo mwa boksi dakika ya 73. Kipa Chove hakuuona kabisa mpira, hivyo kubaki amesimama tu wakati ukitikisa nyavu.
JKT Ruvu hawakuwa na mbinu mbadala ya kuipenya ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Yondani na Cannavaro kwani waliizidi kwa kiasi kikubwa Yanga hasa kipindi cha pili.
Jabir Aziz aliifungia JKT Ruvu goli kwa shuti kali la umbali wa takriban mita 25 dakika 89.
Kocha wa Mbrazil Marcio Maximo alisema baada ya mechi hiyo: "Tunapaswa kupongezana kwa ushindi lakini tuna kazi ya kusahihisha makosa kabla ya kuwavaa Simba. Tunawaheshimu Simba na ninaamini itakuwa mechi ngumu. Hakika itakuwa mechi nzuri lakini mpira wa miguu ni mchezo wa makosa."
Vikosi vilikuwa: Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Edward Manyama, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twute, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santos, Andrey Coutinho na Simon Msuva.
JKT Ruvu: Jackson Chove, Ramadhani Shamte, Napho Zuberi, Madenge Ramadhani, Mohamed Faki, George Minja, Naftali Nashoni, Jabri Aziz, Idd Mbaga, Reliant Lusajo na Gido Simon.