come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA>>>NI MAPEMA MNO KUANZA KUMLAUMU MAXIMO



Na Fikiri Salum

TAYARI kelele zimeanza kujitokeza kuhusu mwenendo wa timu ya Yanga hasa baada ya kupokea kipigo cha pili kutoka kwa Kagera Sugar ya Bukoba.

Yanga ilipata kipigo hicho katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, hicho sasa ni kipigo cha pili baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Yanga inakamata nafasi ya nne ikiwa na pointi zake 10, Mtibwa Sugar yenyewe ndio inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 13, Mtibwa imeshinda mechi nne na kutoka sare mbili.


Coastal Union ya Tanga ikashika nafasi ya pili wakati Azam FC inakamata nafasi ya tatu, Simba miongoni mwa klabu kongwe kabisa hapa nchini inashika nafasi ya tisa baada ya kuambulia sare mechi zake zote ilizocheza.

Simba imecheza mechi sita na hadi sasa ina pointi sita, tayari klabu hiyo imeingia katika mgogoro mzito na imeanza kuwatuhumu wachezaji wake ambapo hadi sasa imewasimamisha
wachezaji watatu kwa makosa tofauti.

Wachezaji hao ni pamoja na Amri Kiemba, Haroun Chanongo na Shaaban Kisiga, Kiemba na Chanongo wamesimamishwa kwa kudaiwa kucheza chini ya kiwango, wakati Kisiga kwa utovu wa nidhamu.

Yanga ambayo ina pointi 10 ikiwa imecheza mechi sita na kushinda tatu kufungwa mbili na ikitoka sare mara moja lakini tayari mashabiki wa timu hiyo wameanza kulalamika chini kwa chini kuhusu mwenendo wa timu yao na kuna uwezekano mkubwa na wao wakaingia kwenye malumbano kama ilivyo kwa hasimu wao Simba.

Wana-Yanga wameanza kumnyooshea kidole kocha wao Mbrazil Marcio Maximo hasa katika upangaji wake wa kikosi cha kwanza na kupelekea timu yao kushindwa kuonyesha soka la
kuvutia.

Ushindi ilioupata Yanga katika mechi zake haujawaridhisha wengi kutokana na ugumu inaokutana nao, Yanga ilizifunga Prisons 2-1, JKT Ruvu 2-1 lakini iliomba mpira umalizike
kutokana na ushindani iliokuwa ikiupata kutoka kwa timu hizo.

Prisons walionyesha kanmdanda zuri na kulishambulia lango la Yanga mara kwa mara kiasi kwamba mashabiki wa Yanga waliomba mpira umalizike ili waibuke na ushindi wao mdogo.

Kocha wa Yanga Marcio Maximo akiwa namsaidizi wake Mbrazil mwenzake Leonaldo Neiva, hadi sasa licha ya kuwezeshwa kila kitu bado Yanga inasuasua lakini ni kutokana na ugumu wa ligi yenyewe hivyo apewe muda zaidi kusuka kikosi 

Mashabiki wa Yanga hawapendezewi na uchezaji wa straika Mbrazil Geilson Santana Santos 'Jaja' ambaye ameshindwa kuwafungia magoli.

Yanga ilienyeshwa na JKT Ruvu na kujikuta ikiomba mpira umalizike ili waweze kuondoka na pointi zote tatu baada ya ushindi wao wa mabao 2-1, vijana wa JKT Ruvu wanaonolewa na mchezaji wa zamani wa Yanga Fred Felix Minziro walionyesha kandanda zuri na kuwazidi ujanja Yanga.

Maximo kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars ameshindwa kuwafanya Yanga kucheza kandanda la kuvutia na kuanza kuwaudhi mashabiki wake.

Lakini hiki si kipindi cha kumlaumu Maximo, ligi bado mbichi mno na Yanga imesaliwa na mechi nyingi ambazo wanaweza kufanya maajabu, sote tunafahamu Maximo tangia anajiunga na timu hiyo tayari amekuta timu iko katika maandalizi ya kuanza msimu mpya.

Muda alioichukua timu na kuanza nayo kazi tayari amekuta programu ya mtangulizi wake ndio imeanza kufanya kazi hivyo itachukua muda mrefu kubadili mfumo, wachezaji aliowakuta wengi wao wamezoea mfumo wa mwalimu mwingine hivyo anapotumia mfumo wake ni ngumu kuuzoea kwa haraka.

Kwa hatua aliyoanza nayo Maximo si mbaya sana kwani hadi sasa timu yake ina pointi 10 na ikiwa katika ushindani mkubwa na vinara wa ligi hiyo, Yanga ya msimu huu licha ya kupoteza mechi mbili lakini ni moja kati ya timu zenye washambuliaji hatari ambao huwekewa mlinzi mkubwa wanaopokutana na timu pinzani.

Tumeona wenyewe jinsi gani mshambuliaji Geilson Santana Jaja ambaye amekuwa akibezwa na wengi kutokana na uchezaji wake wa taratibu lakini ndiye mshambuliaji anayechungwa zaidi na timu pinzani, hapo unaweza kujiuliza kiudogo iweje mchezaji anabezwa kiasi hicho lakini ndiye anayelindwa zaidi uwanjani.

Katika mchezo kati ya Yanga na Simba pamoja na timu nyinginezo Jaja amekuwa akichungwa na zaidi ya mabeki wawili, lakini mchezaji huyo anayetumia zaidi akili kuliko na nguvu kidogo amekuwa akiwatoka na kujaribu kumfikia mlinda mlango.

Kikosi cha Yanga kikiwa kimesheheni wachezaji bora ambao kila kocha angependa we na kikosi kama hicho, lakini hadi sasa kimepoteza mechi mbili na kuanza kuwatia wasiwasi mashabiki wake

Ikumbukwe Simba walimpa umaarufu mkubwa kipa wao wa akiba Peter Manyika Jr kwa sababu ya kuzuia michomo ya Mbrazil huyo, ina maana bila Jaja kipa huyo asingepata misukosuko yoyote.

Jaja alikuwa katika ulinzi wa mabeki wawili ambao walipewa jukumu maalum na kocha wao Mzambia Patrick Phiri kuhakikisha mshambuliaji afurukuti, Jaja aliwaonyesha kuwa yeye ni mchezaji wa kimataifa pale alipofunga magoli mawili ya kistadi zaidi wakati timu yake ya Yanga ilipoibamiza Azam FC mabao 3-0 katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii iliyofanyika Septemba 14 mwaka huu.

Bado Wana-Yanga mnatakiwa kuwa na subira hata kikosi chenu kitapoteza mechi nne au tano, ligi ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa na hasa inatokana na msimu uliopita timu ya Azam FC kuchukua ubingwa wa bara hivyo na timu nyingine zionyesha kuwa zinaweza kushindana na vigogo vya soka nchini ambavyo ni Simba na Yanga.

Mafanikio ya Mbeya City kushika nafasi ya tatu katika ligi iliyopita nayo ni sababu ya kuzifanya klabu nyingine kuonyesha ushindani ili kufikia mafanikio kama hayo ya Mbeya City na Azam FC.

Kingine kinachochangia kuongeza ushindani ni udhamini mnono unaotolewa na Vodacom, Azam TV na Bin Slum Tyres ambao wamekuja kuleta changamoto nyingine kwa wadhamini wa ligi hiyo, 0755 5255216.