come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

NDUMBARO AMEMWONDOA MWAKIBINGA BODI YA LIGI

Sakata la Damas Ndumbaro na Shirikisho la Soka nchini (TFF), linadaiwa kumuachisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Silas Mwakibinga, imefahamika.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa kilichomponza Mwakibinga ni kutokana kufanya kazi kwake kwa weledi na kukataa kutekeleza matakwa ya viongozi wa shirikisho hilo.

Habari ambazo Staa wa leo imezipata jijini jana kutoka kwa chanzo chetu ndani ya TFF, zinaeleza kuwa Mwakibinga alikuwa
ni kiongozi anayefanya kazi kwa kufuata taratibu, kanuni na kuheshimu taaluma yake, hivyo kuonekana kuwa kikwazo pale alipotakiwa kutekeleza maagizo ya viongozi wa TFF waliotaka kila kitu kujibiwa 'ndiyo mzee'.


Chanzo hicho kilisema kwamba kuondoka kwa Mwakibinga katika bodi ni muendelezo wa safari za waajiriwa wa TFF ambao hawatekelezi matakwa ya viongozi wa juu wanaotaka shughuli kufanywa kwa matakwa yao kinyume na kanuni.

Alisema Mwakibinga alikuwa ni kiungo kati ya TFF na Bodi ya Ligi, hivyo kuondoka kwake huku msimu wa ligi ukiwa umeanza, utachangia kurudisha nyuma baadhi ya programu alizokuwa anazifanyia kazi au ameziandaa kutoka kwenye ligi zilizoendelea na nchi nyingine.

"Athari mojawapo baada ya kuondoka kwa Mwakibinga ni kuwa kiongozi atakayekuja atakuwa ni yule anayesikiliza na kufanya kile anachoambiwa kwa kifupi 'Ndiyo Mzee',” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa Mwakibinga alishinikizwa kuachia ngazi na kwamba maamuzi hayo yatarudisha nyuma gurudumu la maendeleo ya soka nchini.

Alisema kwamba soka la Tanzania sasa hivi linazingirwa na vita na ugomvi hivyo suala la kusonga mbele bado ni ‘kitendawili’.

“Sehemu yenye vita na ugomvi, soka haliwezi kuendelea, hiyo hali ndiyo inatuumiza Watanzania kwa sasa,” aliongeza.

Chanzo chetu kilizidi kudai kuwa sababu nyingine iliyomuondoa ofisa huyo ni kukataa kuidhinisha kiasi Sh. milioni 100 za udhamini wa Azam Media ambazo Yanga walizikataa kupelekwa TFF kwa ajili ya matumizi mengine ya shirikisho hilo.

Pia uaminifu wa kiongozi huyo ulionekana ni kikwazo pale alipotakiwa kutekeleza maamuzi ya shirikisho lakini alikwama kutokana na viongozi wengine wa bodi kuwa na msimamo tofauti.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba, baada ya TFF kuingia katika malumbano na Klabu za Ligi Kuu kupitia bodi hiyo kuhusiana na makato ya asilimia tano, Kamati ya Utendaji ilitaka kuivunja bodi na kurejesha usimamizi wa ligi kwa sekretarieti.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya kuona hilo haliwezekani kwa sasa na litautia  'doa' uongozi wa TFF, iliamua kumshitaki Mjumbe wa bodi hiyo na wakili wa klabu za Ligi Kuu, Ndumbaro na hatimaye kufungiwa kujihusisha na soka na kumtaka Mwakibinga ajiuzulu nafasi yake.

Kiliongeza kuwa tofauti kati ya TFF na Bodi ya Ligi ilianza kuonekana baada ya viongozi wa bodi kukataa kusaini fedha kuliazima shirikisho hilo huku ikidaiwa kutajwa kwamba kuna tofauti binafsi zinazosababisha kutokuelewana kwa pande hizo mbili.

"Ni busara ndiyo zimetumika mpaka leo hii bodi ya ligi inaendelea kuwepo, yaani kwa hali ilivyofikia, vyombo hivi vimekua adui badala ya kushirikiana kama ilivyotarajiwa huko nyuma kabla ya kuanzishwa," alisema kiongozi mmoja wa TFF.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwakibinga, alisema kuwa aliamua kuandika barua ya kuacha kazi kutokana na 'maneno' yaliyopo ambayo hakutaka kuyaweka hadharani kwa sasa.

Mwakibinga alisema kwamba ameamua kuachia nafasi hiyo na sasa ataelekeza nguvu katika shughuli zake binafsi."Nimeamua kujiuzulu ili nikafanye mambo yangu, maneno yamezidi kuwa mengi," alisema kwa kifupi Mwakibinga.

TAMKO LA TFF

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura, alisema jana mchana kuwa Mwakibinga ameondoka katika bodi hiyo baada ya kumaliza mkataba wake tangu Oktoba 31, mwaka huu.

Wambura alisema TFF na TPLB wanamshukuru Mwakibinga kwa mchango wake kwa kipindi ambacho ameitumikia bodi hiyo na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya huko aendako.

TPLB hivi sasa iko katika mchakato wa kupata Ofisa Mtendaji Mkuu mpya kwa ajili ya kuziba nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mwakibinga baada ya muda wa mkataba wake kumalizika.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kwamba Mwakibinga hakuwa na mkataba wowote na katika ajira yake hiyo ilikuwa ni ya kuduma tofauti na TFF ilivyotangaza.