Baada ya kutangaza kumtema katika kikosi chao cha Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, uongozi wa Yanga umesema kwamba utamshitaki aliyekuwa kipa wao, Juma Kaseja, katika Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana na gazeti hili, Ofisa Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa kutangaza kumtema ilikuwa ni jambo la kwanza na kinachofuata ni kumshitaki kipa huyo katika kamati hizo zinazosimamia soka Tanzania.
Muro alisema pia Yanga imepanga kumshitaki Kaseja katika mahakama za kawaida za nchi kwa sababu kuna baadhi ya makosa aliyofanya hayahusiani na soka peke yake.
"Tunajipanga kuandaa malalamiko kwenda katika Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji, hatutaishia kumtema tu," alisema Muro.
Aliongeza kuwa Yanga inachukua maamuzi hayo ili kuhakikisha kwamba wachezaji pia wanaheshimu mikataba yao na isionekane kwamba klabu ndiyo zimekuwa na tabia ya kuonea wachezaji.
Alisema baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Yanga leo itafanya mazoezi mepesi kwenye uwanja wao wa Kaunda na kesho itaelekea Bagamoyo kuweka kambi.
Aliongeza kuwa sekretarieti iko katika hatua za mwisho za kuandaa barua na kuipeleka TFF ili kuomba ruhusa ya kuelekea Zambia kushiriki kwenye mashindano maalumu waliyoalikwa.
Yanga ilitangaza kumuacha Kaseja na kueleza kuwa inamdai kipa huyo wa zamani wa Simba na timu ya Taifa (Taifa Stars) fidia ya Sh. milioni 340.
Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh, hakuweza kupatikana jana ili kueleza msimamo wa mchezaji huyo ambaye yuko nje ya timu tangu mwaka jana.