come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KOCHA PLATINUM ASEMA, YANGA NI TISHIO AFRIKA

Yanga imethibitisha ni habari nyingine msimu huu katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya jana kujisafishia njia ya kusonga hatua inayofuata kwa kuichapa Platinum ya Zimbambwe mabao 5-1.

Kipigo hicho kimemfanya Kocha wa Platinum ambaye pia aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Norman Mapeza, kutamka bayana: "Kihisabati tumetolewa mashindanoni lakini kimpira bado tuna nafasi."  

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuhitaji sare yotote ama kutokubali kufungwa zaidi ya mabao 3-0 katika mechi ya marudiano wiki mbili zijazo nchini Zimbabwe ili kusonga mbele. 


Katika mechi hiyo iliyoanza kwa timu zote kusomana, iliwachukua Yanga dakika 31 kuandika bao la kwanza kupitia kwa Salum Telela ambaye alimpiga kanzu kipa wa Platinum, Petro Mhari, hivyo kuwainua vitini mashaki wachache wa timu yao waliojitokeza kuangalia mechi hiyo jana. 

Shuti la dakika ya 41 la Mrisho Ngasa ambalo lilitemwa na kipa Mhari, lilimaliziwa vema kwa mguu wa kulia langoni mwa Platinum na Haruna Niyonzima 'Fabregas' hivyo kuiandikia Yanga bao la pili.

Mabadiliko yaliyofanywa na Platinum dakika ya 44, kwa Wellington Kamudariwa kumpisha Simon Shoko, yalizaa matunda baada ya mshambuliaji Walter Musoma kuihakikishia timu yake haiendi mapumziko katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza kwa kupiga faulo kiufundi ambayo ilimshinda kipa wa Yanga Ali Mustafa 'Barthez' na kujaa nyavuni.

Faulo hiyo iliyopigwa kutoka nje kidogo ya boksi, inamfanya Barthez kufungwa bao la tano katika mechi nne mfululizo za michuano yote.

Kipindi cha kwanza kilimazika takwimu zikiwa zinaonyesha Yanga ilipiga mashuti 4-1, kuotea 2-0, kona 3-2, njano 0-0 na nyekundu 0-0.

Yanga ilianza kipindi cha pili kwa shambulio la kushtukiza kwa mshambuliaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Amissi Tambwe kuitendea haki krosi murua ya dakika ya 46 kutoka kwa Ngasa ambaye alipokea pasi kutoka kwa Simon Msuva na kukimbia na mpira kabla ya kumpasia mfungaji.

Ngasa alirudi langoni kwa Platinum kwa kupiga shuti lililogonga besela na kujaa nyavuni wakati huu akiitendea haki krosi ya Juma Abdul katika dakika ya 24, hivyo kuifanya Yanga iwe mbele kwa mabao 4-1.

Wisdom Mtasa alimpisha Aron Katege dakika ya 60 huku dakika sita baadaye Musoma nusura aipatie Platinum bao la pili, lakini shuti lake la faulo lilikosa macho na kugonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.

Mabadiliko yaliofanywa na Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, katika dakika ya 67 kwa kumtoa Simon Msuva ambaye alimpisha Mliberia Kpah Sherman wakati dakika 10 baadaye Juma Abdul akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Said Dilunga, yalizaa bao kwa Wanajangwani hao.

Alikuwa ni Ngasa tena aliyeifungia timu yake bao la tano katika dakika za majeruhi (90+1) baada ya kuugusa kidogo tu mpira wa krosi kutoka kwa mtokea benchi, Mliberia Sherman.

Bao hilo linamfanya Ngasa ambaye msimu uliopita aliongoza kwa ufungaji kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kufikisha mabao matatu msimu huu sawa na Tambwe ambaye alifunga mawili dhidi ya BDF XI kwenye Uwanja wa Taifa waliposhinda 2-0.

Ngasa alifunga ugenini kwenye Uwanja wa SSKB Lobatse, Botswana wiki mbili zilizopita wakati wakilala 2-1.

Baada ya mechi hiyo kumalizika, Pluijm aliuambia mtandao huu kuwa ushindi huo umetokana na wapinzani wao kufunguka kwa kucheza mfumo wa 4-2-3-1 ikawa rahisi kwao kufunga kwa kutumia mawinga.

"Kwa ujumla ni timu nzuri ambayo inaweza kufanya lolote la maana uwanjani," alisema Pluijm.

Naye Tambwe, akizungumzia ushindi huo, alisema ni kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wa Yanga baada ya kuangukia kichapo kutoka kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu.

Kwa upande wa Mapeza, kocha wa Platinum, alisema kihisabati wametolewa mashindanoni lakini kimpira bado wana nafasi huku akibainisha kuwa Yanga ni timu nzuri inayocheza kwa ushirikiano mkubwa.

"Hali hali ya hewa ya joto pia ilichangia kukiathiri kikosi changu," aliongeza kocha huyo.

Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Calvin Yondan, Said Juma, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngasa na Simon Msuva.

Platinum: Petro Mhari, Raphael Muduviana, Kelvin Moyo,  Gift Bello, Thabani Kamusoko, Wellington Kamudyariwa, Wisdom Mtasa, Brian Muzondiwa, Obrey Ufiwa, Walter Musoma na Elvis Moyo.